Na Fadhili Abdallah,Kigoma
ELIMU ya ujasiriamali na uwekaji wa fedha kupitia vikundi vya kuweka na kukopa kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini imeelezwa kuleta mabadiliko kwa walengwa ambao wameweza kuitumia elimu hiyo kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa ajili ya kuongeza kipato kwa familia.
Hayo yamebainika katika ziara ya kutembelea na kuzungumza na wanufaika wa mpango huo katika halmashauri ya wilaya Kigoma ambao wameeleza kuwa fedha kidogo walizokuwa wakipata wakati wa uzalishaji wameweza kuzitumia kuanzisha miradi.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo kutoka Kijiji cha Nyabigufa Kata ya Mkongoro halmashauri ya wilaya Kigoma walisema kuwa baada ya kuanza kupokea fedha kutoka TASAF walipewa elimu pia ya ujasiriamali na utunzaji fedha kupitia vikundi vya kuweka na kukopa ambapo walianza kukopeshana kuimarisha biashara zao.
Mmoja wa wanufaika hao, Esther Simon alisema kuwa baada ya kuanzaia kupokea fedha katika awamu ya pili ambayo imeendelea hadi awamu hii ya tatu aliwekeza fedha kidogo baada ya kutimiza mahitaji ya msingi akaanzisha biashara ndogo ndogo na baadaye kununua shamba ambapo amenzisha kilimo cha mahindi na maharage.
Naye mohsin Jaffari alisema kuwa baada ya kuwa anapokea fedha kutoka TASAF aliwekeza ili kuanzisha mradi wa kiuchumi baada ya kupata elimu ya ujasiriamali lakini kuelezwa kuwa mpango huo unaweza kufika mwisho hivyo wajiandae kuwa na miradi yao itakayowaingizia kipato.
“Kwa sasa nina shamba la michungwa ambalo lina miti 100 na imeshakuwa na nimeanza kuuza huu ukiwa msimu wa pili, nimeanzisha pia ufugaji wa kuku kwa kuanza na kuku watano na kwa sasa ninao kuku 15, hivyo kwangu naona elimu tuliyopata imetusaidia kuanzisha miradi,”Alisema Mnufaika huyo.
Akizungumzia hilo Mratibu wa TASAF katika halmashauri ya wilaya Kigoma, Jumanne Raphael alisema kuwa wakati walipoanzisha kutoa fedha kwa walengwa wa kaya maskini walikuwa pia wakitoa elimu ya namna ya kuzingatia matumizi ya fedha hizo katika mambo yaliyokusudiwa.
Sambamba na hilo Raphael alisema kuwa pia walitoa elimu ya ujasirimali na utunzaji fedha kupitia vikundi ambapo wanufaika walianza kuwekeza kidogo kidogo na kukopeshana huku maafisa ugani na maendeleo ya jamii wakitoa elimu ya kuanzisha miradi hasa kilimo na ufugaji.
“kwa sasa wanufaika wengi wana miradi ya kiuchumi kwa maana elimu waliyopewa imekuwa na tija na manufaa kwao na hiyo ndiyo mpango wenyewe wa kuwaondoa walengwa hao kwenye umasikini,”alisema Jumanne.
0 Comments