NA MWANDISHI WETU, KATAVI
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Kituo cha Naliendele ya mkoani Mtwara wamewataka wakulima kufuata ushauri wa watalaamu wa zao la karanga ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Akizungumza na wananchi wa vijijiji vya Nsimbo, Kanoge, Mtapenda, Isinde na Uruwira vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mtafiti wa zao la Karanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI kituo cha Naliendele Juma Mfaume ambapo amewataka kulima kitaalamu.
Alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya mbegu aina 17 zimesambazwa kwa wakulima ili kuwezesha kufanya majaribio katika mikoa ya Katavi, Tabora, Kigoma, Geita, Mwanza, Mara na Dodoma.
“Tumetoa mbegu aina 17 kwaajili ya majaribio ambapo zimeenda kwa wakulima wa vijiji mbalimbali ambapo tunafanya tafiti shirikishi katika mikoa hiyo ili kubaini ipi mbegu bora itakayowafaa wakulima wa zao la karanga ndani ya Wilaya hiyo” alisema Mfaume
Nae Afisa Kilimo Kata wa Kata ya Mtapenda Stephenia Chiza alisema kuwa wakulima wengi wameitikia na wamefanya majaribio hayo katika mashamba yao.
“Unajua karanga ni zao la biashara wakulima wengi wananufaika kwa kulima zao hilo utolewaji wa elimu kwao utaongeza hamasa zaidi ya kulima zao hilo na kuwaletea maendeleo makubwa”
“Wakulima wengi walikuwa wakihangaika na magonjwa, wadudu ukame ukipita wanakosa mavuno lakini sasa uwepo wa hizi mbegu utafutungua ukurasa mpya kwa wakulima wa kata hii na kuwainua kiuchumi” alisema Chiza
Nae Joseph Golya mkulima kutoka kijiji cha Mtapenda C alisema kuwa amekuwa akilima zao hilo kwa muda mrefu ambapo kwa sasa ameweza kupata mbegu ambazo zimeleta majibu zaidi.
“Unajua mbegu za asili hushambuliwa na ugonjwa wa ukoma hii imekuwa ikikatisha sana tamaa wakulima kulima zao hilo ambapo ujio wa mbegu bora umehamasisha wakulima kulima alipewa kilo nne za karanga”
Nae Thomas Kabanda mkulima wa kijiji cha Uruwira halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi alisema kuwa ujio wa mbegu bora umeongeza hamasa ya wakulima wa kijiji hicho kulima karanga kwa wingi.
“Hizi mbegu bora zina karanga nzito kubwa nene zina mafuta mengi yaani ukiingiza sokoni hakuna ubishi wa kupata soko hii inatupa hamasa ya kulima zaidi”
0 Comments