KUFUATIA kila mwaka hekari 400,000 za miti kupotea nchini kutokana na matumizi mbalimbali ya miti Kampuni ya Taifa Gesi imeandaa shindano kwa waandishi wa habari nchini ili kuhamasisha jamii matumizi ya nishati mbadala ya gesi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa kampuni ya gesi Anjela Bhoke kwenye shule ya sekondari Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala kwa mkoa wa Pwani uliyoandaliwa na benki ya NMB, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jafo.
Bhoke alisema kuwa wameandaa shindano kwa waandishi wa habari na kuwatunukia kwani wanatumia talanta zao kwa kuelimisha umma matumizi ya gesi ambayo ni safi na salama.
Katika hatua nyingine Benki ya NMB wametenga kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya shule zitakazopanda miti 2,000 na kuitunza kwa asilimia 80 ambapo itapatiwa milioni 50, huku mshindi wa pilia kwa kupanda miti 1,500 akipata milioni 30 akiitunza kwa asilimia 70 na watatu akipata milioni 20 kwa kupanda miti 1,000 itakayokuwa imetunzwa kwa asilimia 70.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa mkoa umeweka mikakati mbalimbali ili kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti million 13.5 lakini hadi sasa wameshapanda miti milioni 9.7 ikiwa ni zaidi ya asilimia 70 ya malengo ni kukabiliana na uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye mkoa huo.
0 Comments