NA THABIT MADAI, ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA APP
TAASISI za kibiashara ikiwemo mabenki na wafanyabiashara zimeshauriwa kutoendekeza kupata faida katika biashara zao katika mwezi mtukufu wa ramadhan na badala yake kutumia mwezi huo kutoa sadaka kwa wasio na uwezo ili kupata radhi za MwenyeziMungu.
Ushauri huo umetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya Watu wa Zanzibar Hussein Migond katika hafla ya kukabidhi misaada ya vyakula katika vituo vya watoto yatima, wajane, wazee na watu wasiojiweza.
Alisema mwezi mtukufu wa ramadhan ni mwezi wa kuchuma thawabu hivyo ni lazima kutoa sadaka zao kwa makundi hayo ambazo zitawaongezea thawabu na kuona jamii inaishi kwa amani na upendo.
Alisema makundi hayo yana uhitaji mkubwa kupata vyakula ambavyo vitawezesha kupata futari kama watu wengine wenye uwezo hasa watoto yatima na wanaoshi katika mazingira magumu.
Aidha alisema benki hiyo ni kawaida ya kila mwisho wa mwaka inapofika mwezi mtukufu wa ramadhan kinachopatikana katika faida ya benki basi wanakirudisha kwa wananchi kupitia misaada hiyo wanayoitoa kwa makundi hayo.
Mjumbe Hussein alisema PBZ ni miongoni mwa benki kubwa Tanzania na imeingia katika nafasi ya benki bora ambapo mafanikio makubwa na mashirikiano ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuisimamia vizuri benki hiyo kwani anataka tasisi zake na mashirika kujiendesha kibiashara na benki hiyo imeitikia wito huo.
Sambamba na hayo alisema PBZ ni walipakodi wakubwa kwa serikali fedha ambazo zinasaidia kuleta maendeleo kwa nchi.
"Faida inayopatikana PBZ asilimia kubwa inakwenda serikalini na tunatoa sehemu ya faida hiyo kuwahudumia wananchi ikiwemo kutoa sadaka kwa makundi mbalimbali kama haya ya watoto yatima, wajane, wazee na makundi mengine", alibainisha.
Hivyo aliwaomba wananchi ambao hawajaitumia benki hiyo kwa kufungua acaunti basi kuitumia na kuiunga mkono ili kuona faida inayopatikana inaendelea kurudi kwa wananchi wa Zanzibar.
"Wananchi waendelee kuiunga mkono benki yao na kuamini kwamba amana zao zipo sehemu salama", alisema.
Mbali na hayo alivitaka viongozi wa vituo hivyo kuhakikisha msaada huo unatumika kwa walengwa waliokusudiwa.
Nao viongozi wa vituo hivyo waliipongeza benki hiyo kwa msaada walioutoa katika maeneo hayo kila mwaka ambao unasaidia kwa kiasi kikubwa makundi hayo kupata futari.
Mkurugenzi Jumuiya ya Wajane Zanzibar, Tabia Makame Mohammed, Mkuu wa kituo cha Kulelea Watoto Mazizini Asha Abeid Masoud, Mkurugenzi wa kijiji cha SOS Asha Salum Ali na Mzee Mtoro Seif anaeishi katika nyumba ya wazee Welezo walisema msaada huo ni chachu kwa mashirika mengine kuiga mfano wa benki kuweza kusaidia makundi hayo na makundi mengine ambayo yana uhitaji.
Hivyo waliiomba benki hiyo isiwe mwisho na badala yake kuendekea kuwasaidia kwani makundi hayo bado yanauhitaji mkubwa.
Benki hiyo imetoa misaada ya vyakula ikiwemo unga wa ngano, mchele, mafuta unga wa sembe kwa wajane, nyumba za kulelea watoto ikiwemo Mazizini, SOS, Assalam Chuo cha Zanzibar Univasity na Maftui Foundation Tunguu na nyumba za Wazee Welezo na Sebleni ambapo inatarajia kutumia milioni 70 kutoa msaada huo kwa makundi hayo Unguja na Pemba.
0 Comments