SERIKALI imeanza kutenga fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu sahihi katika eneo la mti mrefu kuliko yote barani Afrika wenye urefu wa mita 81.5 uliopo kijiji cha Tema ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro ili watalii waweze kufika kwa urahisi.
Kauli hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Utalii, Mery Masanja kuwa mti mrefu kuliko yote barani Afrika upo katika msitu wa Mlima Kilimanjaro katika kijiji cha Tema miundombinu ya kufika katika eneo hilo na mazingira ya eneo ni mabaya je Serikali inamkakati gani wa kuboresha eneo hilo ili kuweza kupata fedha za kigeni.
Prof. Ndakidemi pia alihoji je Serikali inampango gani wa kufungua VIP route ya Kidia ambayo hupeleka watu maarufu kupanda mlima Kilimanjaro na kujipatia fedha za kigeni kama walivyokusudia.
Akijibu swala hilo, Naibu Waziri wa Utalii Mery Masanja alisema, Serikali wameshaa kutenga fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu sahihi katika eneo hilo na mti mrefu ambapo mchakato huo utaanza mwaka wa fedha.
Mery alisema kuwa, kwa sasa Wizara imeshaanza ukarabati wa lango la VIP route lipo asilimia sabini na kwa sasa wanatafuta wawekezaji kwa ajili ya kujenga huduma za malazi na chakula.
"Mwaka wa fedha 2023/24 tutajenga lango kuu linalopitia katika VIP route ambalo litasaidia wageni kuingia katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro" alisema Naibu Waziri Mery.
Alisema kuwa, Serikali imeendelea kuweka kipaombele na jitihada katika ukarabati wa barabara zinazotumika kupeleka watalii katika mlima Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mamlaka husika za ukarabati wa barabara.
Aliongeza kuwa, miongoni mwa jitihada hizo zilizotumika ni pamoja na ujenzi wa barabara za Machame, Mweka na Marangu kwa kiwango cha lami pamoja na ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za changarawe zinazoelekea lango la Rongai, Lemosho, Kilema, Londolosi na Umbwe.
Alisema kuwa, mwaka wa fedha 2023/24 Serikali itafanya ukarabati kwa kiwango cha changarawe kwa barabara inayoelekea kwenye lango la Umbwe.
Mwisho.
0 Comments