Mkuu wa Polisi wilaya ya Iringa na mkuu wa kikosi Cha usalama barabarani wilaya hiyo wamefanya msako mkali wa madereva wanaokiuka sheria za usalama Barabarani.
Pamoja na Msako huo Madereva wameonywa kuacha tabia ya Kukaidi sheria za Usalama Barabarani .
Lengo la Msako huo likiwa ni kuhakikisha wanatoa elimu na usimamizi wa hali ya juu kudhibiti na kupunguza ajali Kuelekea sikukuu za EID
Akizungumza na Abiria pamoja na Madereva wa Mabasi katika Stendi kuu ya Iringa iliyopo Igumbiro, SSP Benard Samara ambaye ni OCD Iringa alisema wakati huo wa Kuelekea sikukuu za EID jeshi hilo linataka Madereva kuzingatia sheria za barabarani .
" Tunaelekea katika kipindi cha sikukuu na kipindi hiki ndio muda ambao shetani naye anajichanganya ili kupoteza uhai wetu. Madereva mnakaidi vyombo vya Usalama Barabarani, tunaongea vizuri hapa lakini abiria wenu wakishawapampu kwamba tunataka tuwahi, mnawasikiliza zaidi abiria zaidi ya Maelekezo tunayowapa kuhusu Usalama Barabarani, kwahiyo chondechonde."
"Madereva mnawahi wapi wakati bado upo ndani ya muda wako wa kuingia stendi au kufika mahala husika. Sikukuu ya Christmas mmepita vizuri, pasaka mmepita vizuri basi na sikukuu zinazokuja mmpite vizuri tusije tukasikia Ajali labda itokee kwa bahati mbaya lakini mtusaidie kwenye hayo magari mnayoyaendesha." - Ni maneno ya SSP Benard Samara ambaye ni OCD Iringa, alipoongea na Madereva Stendi kuu Igumbiro Iringa.
Naye Mkuu wa Usalama wa Barabarani wilaya ya Iringa , ASP Glory C. Mtui (DTO Iringa), alisema "Tunasisitiza utii wa sheria bila kushurutishwa, haijarishi askari yupo Barabarani ama hayupo unapaswa kutii alama zilizopo Barabarani, unatakiwa uzingatie ukomo wa mwendo kasi, lakini pia kutokana na kwamba sikukuu hizi zinaangukia mwisho wa juma, madereva msizidishe abiria kwenye magari yenu.
Sisi tutaendelea kuwaangalia kwa kutumia tochi na mifumo yetu ya VTS, msitumie vilevi maana tutawapima na tuna vipima ulevi vya kutosha"
Abiria wameombwa kuwa walimu wa kwanza kwa madereva pindi wanapopanda gari na kumuona dereva anaendesha gari kwa mwendo kasi bila kuzingatia taratibu za usalama Barabarani kwani kufika salama uendako ndio lengo kuu la safari hivyo Bora kuchelewa lakini umefika Salama.
0 Comments