Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wameingia mkoani Kigoma kuomba hifadhi ya ukimbizi imefikia 6021 huku idadi hiyo ikipungua ukilinganisha na wiki mbili zilizopita ambapo waomba hifadhi hao walianza kuingia nchini.
Mratibu wa idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi kanda ya Magharibi, Nashon Makundi alisema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari akielezah maendeleo ya wakimbizi wa DRC ambao wameendelea kuingia nchini.
Akieleza mtiririko wa waomba hifadhi hao kuingia nchini Makundi alisema kuwa hadi sasa waomba hifadhi 6021 wamepokelewa na kuandikishwa ambapo kati yao zaidi ya 3000 tayari wameshapelekwa kwenye kambi ya wakimbizi wa DRC ya Nyarugusu iliyopo Kasulu mkoani Kigoma.
" kwa sasa idadi ya waomba hifadhi wanaoingia nchini imepungua kukiwa na wastani wa waomba hifadhi 100 hadi 200 wanaoingia ukilinganisha na waomba hifadhi 600 waliokuwa wakiingia hapo awali na kwamba wanaoingia taratibu za kuwahoji kupata taarifa zinaendelea kama kawaida,"Alisema Mratibu huyo wa wakimbizi.
Katika hatua nyingine Makundi alisema kuwa Watanzania 50 ambao walijiorodhesha kama sehemu ya waomba hifadhi ili kupewa hadhi ya ukimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamenyimwa hadhi ya ukimbizi na kurudishwa majumbani kwao.
Makundi alisema kuwa Watanzania hao wana mahusiano ya kifamilia na wakimbizi hao wa DRC hivyo taratibu za nchi haziwezi kuwaruhusu kuishi kambini kama wakimbizi wakati wanayo miji yao waliyokuwa wakiishi kabla ya kuingia kwenye mahusiano.
Alibainisha kuwa baadhi ya Watanzania hao hawana nyaraka (vyeti vya ndoa) kuwathibitishia uwepo wa ndoa baina yao na wenzao hao wa DRC hivyo bado taratibu za kuwapa hadhi ya ukimbizi na kuishi kambini kwa maana ya kuwafuata wake au waume zao hazikubali.
Baadhi ya wakimbizi wa DRC walioongea na waandishi wa habari wameeleza hali tete ya usalama ilivyokuwa na kulazimika kukimbia na kuomba hifadhi nchini Tanzania.
Mmoja wa waomba hifadhi hao,Alaki Tulale kutoka Butembo jimbo la Kivu ya Kusini alisema kuwa amekimbia baada ya kuvamiwa na waasi wa M23 kwenye makazi yao ambao wamekuwa wakiteka vijana na kuwataka kujiunga na kambi zao sambamba kuua watu.
Alisema kuwa nyumbani kwao mkoa Fizi ambako wazazi wake na ndugu zake walikuwa wakiishi hali ni mbaya na hajui hadi sasa ndugu zake wana hali gani lakini anashukuru yeye binafsi yuko salama hapa nchini.
Kwa upande wake Mabiso Kundukilo kutoka mkoa Baraka alisema kuwa vita imekuwa kubwa kwao na watu kutekwa sambamba na kuuawa akiwemo mume wake ambaye alichukuliwa nyumbani na hadi sasa hajuia yuko wapi.
0 Comments