Header Ads Widget

WADAU WATAKA USHIRIKISHWAJI MKUBWA WA MADHEHEBU YA DINI VITA DHIDI YA UKATILI

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

WADAU wa kupinga ukatili mkoani Kigoma wamesema kuwa madhehebu ya dini yanayo nafasi kubwa katika kubadilisha jamii kukabili vita dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto.


Padri Castus Rwegoshora kutoka kanisa Katiliki jimbo la Kigoma alisema hayo akitoa mchango wake kwenye mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kupinga ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWA) na kusema kuwa bado madhehbu ya dini hayajatumika kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huo.



Moja ya mambo ambayo kiongozi huyo wa dini alisema kuwa ni kitendo cha wazazi kushindwa kuyapa umuhimu mafundisho ya dini kwa watoto wao  mambo ambayo ndiyo msingi wa kuwawajenga kiimani na kuwa na moyo na vitendo ambavyo havihusiani na ukatili wanapokuwa wakubwa.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Promotion Centre (WPC), Martha Jerome alisema kuwa madhehebu mbalimbali ya dini yakipewa nafasi kubwa ya kusimamia malezi ya watoto na kutoa nasaha kwa jamii kila wakati inaweza kusaidia kupunguza hali ilivyo sasa na watu kuishi kwa hofu ya Mungu.




Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa dawati la jinsi la jeshi la polisi mkoa Kigoma,Michael Mjema alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa madawati hayo na kuanza kutekelezwa kwa MTAKUWA kumekuwa na mafanikio makubwa kwa jamii kutoa taarifa kwa matukio ya ukatili yanayotokea na kuwezesha mamlaka mbalimbali kuchukua hatua.



Hata hivyo Mjema alisema kuwa bado wazazi na familia zimekuwa kikwazo kwa mashauri mengi kushindwa kufika mwisho na watuhumiwa kushindwa kuchukulia hatua kutokana na familia kukaa kulimaliza shauri hilo nyumbani na wakati mwingine kuharibu ushahidi au kushindwa kutokea kabisa mahakamani kesi inapofikishwa huko.



Akifunga mkutano huo wa siku moja wa wadau wa kupinga ukatili mkoani humo kutathimi utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili (MTAKUWA) Katibu Tawala wa mkoa Kigoma Albert Msovella alisema kuwa hali bado ni mbaya na wadau wote wanapaswa kuungana kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili.



Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa wilaya Buhigwe mkoani Kigoma,Peter Masindi alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika utekelezaji wa MTAKUWA lakini hali ya ukatili nchini na mkoa Kigoma bado mbaya.



Katibu Tawala huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kubeba ajenda ya jambo hilo kama jambo lake binafsi katika kuwalinda watoto na wanawake huku akitoa rai kwa wazazi katika kuhakikisha ulinzi na matunzo ya watoto wao.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI