Na Fadhili Abdalla,Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimewataka watanzania nchini kote kutumia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuwataka kutokubali maneno ya kejeli yanayobeza utekelezaji wa miradi hiyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma,Jamal Tamim alisema hayo akizunguumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanaj wa Community Centre mjini Kigoma na kusema kuwa miradi hiyo inatija kubwa katika maisha ya kila Mtanzania.
Alisema kuwa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi wa umeme wa bwawa la Nyerere, reli iendayo kasi (SGR),uboreshaji wa miundo mbinu ikiwemo miradi mikubwa ya barabara na madaraja ambayo yote kwa kiasi kikubwa inalenga kuleta unafuu wa maisha na kukuza uchumi wa mtanzania mmoja mmoja wakiwemo wale wa kipato chini.
Mwenyekiti huyo alitoa mfano wa miradi inayofanyika mkoani Kigoma ikiwemo ujenzi wa daraja la Kikwete, barabara za kiwango cha lami ambazo zimeuwezesha mkoa huo kufunguka na watu wote kufanya shughuli zao kwa urahisi na kuwezesha watu wengi kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano huo Mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Gisuru mkoa Ruyigi nchini Burundi, havyarimana Silasi kutoka cha tawala cha CNDD-FDD ambaye alikaribishwa na kuzungumza kwenye mkutano huo alisifu jinsi Tanzania inavyoendesha siasa zake na kuwapa uhuru vyama vyote kufanya kazi zao kwa misingi ya demokrasia.
Havyarimana alisema kuwa serikali ya Burundi na Chama Tawala cha CNDD-FDD kinajifunza mambo mengi ya uendeshaji wa nchi na chama chao kutoka serikali ya Tanzania na CCM na kuifanya Burundi kufikia ilipo sasa na kuondokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibondo, Hamisi Tairo alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Raisi Samia Suluhu Hassan mkoani Kigoma ikiwemo miradi ya barabara za lami zenye urefu wa zaidi ya kilometa 260 huku wilaya hiyo ikipata barabara ya ziara kutoka Kibondo mjini kuelekea Mabamba mpakani na nchi ya Burundi.
Tairo alisema kuwa miradi hiyo inatija kubwa kwa wananchi wa mkoa Kigoma katika kukuza uchumi na kuondoa umasikini jambo linaloufanya mkoa huo kuachana na historia ya mkoa huo kutengwa lakini pia kuwa mwisho kwa umasikini.
0 Comments