Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati msimu wa mavuno ya parachichi ukiendelea katika mikoa mbalimbali hapa nchini na mataifa mengine na kuwaingia mamilioni ya fedha za kigeni wakulima,Kumeripotiwa kuibuka kwa wimbi la matapeli wanaotumia kampuni za watu wengine kuwaibia wakulima matunda hayo.
Miongoni mwa kampuni inayoonekana jina lake kutumiwa na matapeli hao ni pamoja na Shikamoo parachichi yenye makao makuu yake mjini Njombe ambapo mkurugenzi wake Erasto Ngole anajitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuonya tabia hiyo na kwamba kuna zaidi ya trei 70 za parachichi walizotapeliwa wakulima hadi sasa.
Aidha Ngole amesema kutokana na malalamiko hayo mpaka sasa amemkamata kijana mmoja ambaye alienda kuchuma parachichi kwa wakulima wa kijiji cha Igosi wilayani Wanging'ombe na kujitambulisha kuwa anatokea kampuni ya shikamoo parachichi.
Kwa njia ya simu nimemtafuta mmoja wa wakulima waliotapeliwa bwana Hassan Mapunda ambaye amekiri kutapeliwa licha ya kupambana nao hadi kuwakamata.
Kituo hiki kimefika katika kijiji cha mfereke kata ya Utalingolo halmashauri ya mji wa Njombe na kufanya mazungumzo na baadhi ya wakulima wa parachichi akiwemo Flouris Mwanyika na Anisethi Ngole ambao wanaonya tabia za baadhi ya vijana wanaoshindwa kujitafutia kipato halali na kujiingiza kwenye utapeli wa parachichi kwa wakulima.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kijiji cha Mfereke Elia Chilatu anasema wamejiwekea mkakati wa kushirikiana kukabiliana na wezi wa parachichi kwa kupeana taarifa za haraka pindi linapotokea tukio lolote mashambani.
Wenyewe wanasema parachichi ni dhahabu ya kijana hivyo kila mmoja anaowajibu wa kuilinda dhidi ya matapeli na wezi wanaochuma fedha kupitia matunda ya wengine.
0 Comments