Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mheshimiwa Sebastian Muungano Waryuba amewafukuza wilayani kwake wakandarasi wawili walioshindwa kutekeleza kazi za miradi ya maji na barabara kwa wakati kulingana na mikataba ya kazi za ujenzi wa miradi ya serikali.
Wakandarasi waliofukuzwa kufanya kazi zozote za ukandarasi wilayani humo ni UK Construction ambae alikuwa anatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara kiwango cha changarawe cha klilomita 8.6 kutoka Lugala kwenda Biro na mkandarasi Wagala ambae alikuwa anatekeleza mradi wa maji Misegese na Itete Njiwa.
Mradi wa barabara ya Lugala kweda Biro unatekelezwa kwa shilingi milioni 910,816,000 ambapo tayari mkandarasi huyo alishalipwa kiasi cha shilingi milioni 215,686,200.
Kulingana na marufuku hiyo mkuu wa wilaya amemtaka mkandarasi ambae alikuwa anatekeleza mradi wa maji kampuni ya Wagala kurejesha kiasi cha shilingi milioni 65 alizolipwa na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU wilayani Malinyi kusimamia urejeshwaji wa fedha hizo ikiwa ni pamoja na kutathmini kazi aliyofanya ya kuchimba shimo kwa ajili ya mradi wa huo.
Akizungumza na wakandarasi wanaofanya kazi za miradi katika wilaya ya Malinyi mkuu wa wilaya amewataka kuzingatia muda wa kazi weledi na uaminifu katika kutekeleza miradi ya serikali.
Mbali na hilo amezitaka mamlaka zote zinatoa kazi kwa wakandarasi kabla ya kuwapa mikataba ya kazi kujiridhisha kuwa wakandarasi hao wana vifaa vya kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Wakandarasi wengi wanaotekeleza miradi hapa kwetu ni wajanja wajanja wanaweka vijana kule site kusikilizia kama kuna lolote linaweza kutokea lakini ukweli hawapo site wanacheza na serikali sasa naagiza wote mliopewa kazi katika wilaya hii muende site na nitakuwa napita kukagua mwenyewe nikikukuta haupo na kazi haifanyiki nitakuondoa katika mradi”alisema Waryuba.
Baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi katika wilaya ya Malinyi waliozungumza katika kikao hicho wameiomba serikali kuwapatia wananchi elimu ya utunzaji wa miradi inayotekelezwa ili kuondoa tatizo la urudia ujenzi wa miradi kutokana na uharibifu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALI-H/W MALINYI
0 Comments