Na Amon Mtega, Mbinga
Baadhi ya Wakazi wa kata Mbinga 'B' pamoja na wafanyabiashara wanaofanyia biashara zao kwenye maeneo ya kituo cha magari ya abiria(Stendi)Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga mji Grace Quintene kwa kukarabati Miundombinu ya kituo hicho .
Akizungumza mmoja wa Wakazi hao ambaye pia ni mfanyabiashara kwenye kituo hicho Faustin Hamis ( Masawe) amesema kuwa kituo hicho Miundombinu yake ilichakaa hasa kwenye vyoo ambapo chemba zote ziliziba lakini kufuatia ukarabati uliofanywa umekifanya kituo hicho kuendelea kuwa bora.
Hamis amesema kuwa chemba za vyoo hizo ambazo ziliziba zote zimefanyiwa matengenezo na kuwa kwa sasa hakuna tena adha inayowakabili wasafiri au Wakazi wa maeneo hayo pindi wanapohitaji huduma ya vyoo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mbinga 'B' Sulutan Andoya amesema kuwa ukarabati huo umefanyika baada Halmashauri ya Mbinga mji kutoa fedha ya kufanyia ukarabati huo na kuwafanya Wakazi wa maeneo hayo na abiria kuendelea kutumia huduma za Miundombinu hiyo.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga mji Grace Quintene amesema kuwa ukarabati wa Miundombinu hiyo umetumia fedha za makusanyo ya ndani na kuwa wataendelea na ukarabati kwenye maeneo yaliyobakia ili kurudisha hadhi ya kituo hicho.
0 Comments