Header Ads Widget

TUMEINGIA KATIKA 'SUK' KWA MASLAHI YA TAIFA - OTHMAN

 





Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema wameingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ili kulinda maslahi ya Taifa na si vinginevyo.


Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo katika salamu zake fupi mbele ya Mkutano wa hadhara wa Chama chake, uliofanyika Viwanja vya Mbagala Zakhiem, Jijini Dar es Salaam.


Amesema kuwa ACT-Wazalendo hawakujumuika kuongoza Serikali ya Zanzibar kwa kufuata vyeo, bali ni kwa azma ya kulinda maslahi ya Tanzania, ambayo yanaguswa moja kwa moja, pindipo kukiwepo migogoro upande wa Zanzibar.


Hivyo, Mheshimiwa Othman aliyeambatana pia na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, katika Mkutano huo, amewataka wafuasi, wanachama na wapenzi wa  Chama hicho, kuamini kuwa,  yeyote anayelaumu uamuzi wa ACT- Wazalendo kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (GNU) ameishiwa na 'bundle' (salio) la kisiasa.


Kiongozi wa  ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Zuberi Kabwe, ameuambia umma katika Mkutano huo, kuwa hawatosita kuendeleza azma ya kuwatetea wananchi sambamba na mambo muhimu, ambayo Chama chake kimeyaandaa kwaajili ya Watanzania.


Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kupaza sauti dhidi ya vitendo vyote vya ubadhirifu nchini; kudai Katiba Mpya; Mabadiliko ya Sheria kandamizi; na kupigania haki za watu mbalimbali waliotendewa dhulma kwa namna moja au nyingine.


Zitto amewataka Watanzania kukiunga mkono Chama hicho ambacho kipo mstari wa mbele kuwatetea na kupigania maendeleo ya kweli,  sambamba na Kaulimbiu ya sasa isemayo, "Taifa la Wote, Maslahi ya Wote'.


Naye, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Bw. Juma Duni Haji, amewaahidi Wananchi na wafuasi wa Chama chake akisema watarajie kuyapata mengi ambayo hawakuyafaidi katika Kipindi chote ambacho sauti zao zilizimwa.


Viongozi mbali mbali wametoa salamu zao katika Mkutano huo, wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, Bi Doroth Semu;  Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ndugu Ado Shaibu; Mwenyekiti wa Vijana wa Chama hicho, Bw. Abdul Nondo; na Waziri Kivuli wa Chama hicho anayehusika na mambo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bi Kulthumu Mchuchuli.


Wengine waliohudhuria hapo ni pamoja na; Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani; Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Bw. Omar Said Shaaban na viongozi wa ngazi mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.


Mkutano huo umekuja kama sehemu ya Ufunguzi wa Mikutano ya Hadhara ya Chama hicho, ambayo kwa ujumla Nchi nzima siasa za namna hiyo zilikabiliwa na zuio, kwa takriban miaka 7 iliyopita.


Mkutano huo ulitanguliwa na matembezi yaliyoongozwa na Viongozi wakuu wa chama hicho yaliyoanzia maeneo ya Mbagala Misheni na kuhitimishwa katika Viwanja vya Mbagala Zakhiem.




Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Februari 19, 2023

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI