Header Ads Widget

TCU KUIMARISHA MIFUMO YAKE YA NDANI ILI VYUO VIKUUVIENDANE NA MWELEKEO NCHI

 


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma


TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)imeendelea kuimarisha mifumo yake ya uthibiti ubora na mifumo ya ndani ya vyuo vikuu ili kuhakikisha vyuo vikuu vinaendana na mwelekeo wa nchi, ambapo Tanzania imelenga kuwa Taifa la watu wenye maarifa, ujuzi, weledi na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake ifikapo mwaka 2025 .


Akizungumza na waandishi wa habari leo Kijiji hapa wakati akiwaeleza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za time hiyo Katibu Mtendaji Profesa Charles Kihampa Amesema mifumo hiyo itathibiti ubora pamoja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na uwepo wa viwanda. 


Amesema katika kuhakiki ubora, TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara, wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda, na kimataifa. 


"Kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa," Amesema


Na kuongeza "Zoezi  hili la ukaguzi wa vyuo ni endelevu kila mwaka vilevile TCU imeweka utaratibu wa kuanzishwa na kuimarishwa mifumo ya uthibiti ubora ndani ya vyuo vikuu ambapo vyuo vyenyewe vimekua na utaratibu wa kujikagua, kujitathmini na kufanya marekebisho mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya uendeshaji wa vyuo vikuu,"Amesema Kihampa



Na kuongeza "kimsingi, mifumo ya ushauri, ukaguzi, na ufuatiliaji wa mara kwa mara imefanya vyuo kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa, mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki, madarasa na kuongeza idadi ya viongozi na wahadhiri wenye sifa stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

 

Amesema  kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.4 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation-HEET) kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo vikuu iko katika hatua mbalimbali za kufanyiwa mapitio ili kuhuishwa kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali ili kukidhi matarajio yao na mahitaji ya soko. 



Katika kufanikisha hili, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa viongozi na wanataaluma wa vyuo vikuu kuhusiana na uendeshaji wa vyuo vikuu, utengenezaji mitaala inayozingatia ujuzi na inayoendana na soko, mbinu za ufundishaji kwa wahadhiri ambao hawakusoma fani za ualimu, ulinganifu wa programu za masomo (programme benchmarks), uthibiti ubora, na utengenezaji na utumiaji wa mifumo ya kompyuta. 


"Kwa mfano, katika kipindi cha  Julai hadi Desemba, 2022 jumla ya viongozi na wanataaluma 575 wameshanufaika na mafunzo hayo ambapo Mafunzo hayo yamelipiwa na serikali kwa asilimia 100.



Aidha Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuongeza wigo wa fursa za masomo ya elimu ya juu kwa watanzania ambapo katika kipindi cha miaka miwili fursa mbalimbali za masomo zimeongezeka.


 Nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu katika programu za Shahada ya Kwanza zimeongezeka kutoka 157,770 mwaka 2020/21 hadi 172,168 mwaka 2022/23 ambalo ni ongezeko la nafasi 14,398 sawa na asilimia 9.1.


  Programu za masomo ambazo zimeruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza zimeongezeka kutoka 686 mwaka 2020/21 hadi 757 mwaka 2022/2023.


 Wanaodahiliwa katika shahada ya kwanza wameongezeka kutoka 87,934 mwaka 2020/21 hadi 113,383 mwaka 2022/23 sawa na asilimia 28.9.


  Idadi ya Wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu imeongezeka kutoka 259,266 mwaka 2020/21 hadi 295,919 mwaka 2021/22 sawa na asilimia 14.1. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka kwa mwaka wa masomo 2022/2023.

 

Hata hivyo, licha ya vyuo vikuu, wadau wengine ambao hadi sasa wamenufaika kutokana mifumo yao kuunganishwa na TCU ili kujipatia taarifa mbalimbali ni pamoja na Wizara ya Afya, na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

 

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI