Header Ads Widget

MSIWATUMIE WALEMAVU KAMA KITEGA UCHUMI

 


Na Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP MOSHI

Jamii imeaswa kuacha kuwatumia watu wenye ulemavu kama sehemu ya kitega uchumi na badala yake kutafuta njia sahihi za kuweza kuwasaidia kutokana na hali waliyonayo.


Hii imetokana na baadhi ya watu kwenye jamii kuwazungusha walemavu mijini wakiomba misaada kutoka kwa wasamaria wema ambapo pia huenda isiwafikie kama ilivyokusudiwa.



Akizungumza mjini Moshi katika sherehe za watu wenye ulemavu rais wa shirika lisilokuwa la kiserikali la New life Foundation (NLF)nchini Dkt Glorious Shoo amesema kumekuwa na kasumba ya watu wenye ulemavu kutumika kama sehemu ya kitega uchumi jambo ambalo sio sahihi 


"Kuna mtu anawachukua hawa ndugu zetu alafu anawapa vibaiskeli na watu wakuwatembeza alafu jioni anawatoza fedha hivyo anajinufaisha kupitia wao"anasema



Dkt Shoo anasema kuwa kwa kutambua umuhimu wa watu hao (NLF)wakiandaa siku hiyo muhimu ikiwa ni jitihada za kuwatambua lakini pia kuwafariji kutokana na hali ya ulemavu waliyonayo


Anasema sherehe hiyo iliyokwenda sambamba na kuwatunuku vyeti ni faraja kwao lakini pia kuikumbusha jamii kuwa ulemavu unaweza kumpata mtu yoyote kwa wakati wowote ule hivyo kama jamii haina budi kutambua mchango wa watu wenye ulemavu waliopo kwenye jamii zetu.


"Haiwezekani mtu ni mlemavu anazungushwa tena kwenye jua Kwa kisingizio cha kuomba msaada lakini naomba kuikumbusha jamii kuwa suala la ulemavu ni suala la dakika moja tu hivyo ni lazima kama jamii sasa tuone umuhimu wa hawa wapendwa wetu"anasema


Aidan Shayo ni mmoja wa watu wenye ulemavu wa uti wa mgongo ambapo alisema sherehe hizo zimewafariji watu wenye ulemavu ambapo pia walikutanishwa kwa pamoja na kuweza kubadilishana mawazo


Anasema watu wenye ulemavu Kwa kipindi kirefu kwenye jamii walionekana kubaguliwa katika mambo mbalimbali lakini kwa sasa hali imebadilika baada ya jamii kujengewa uelewa


"Hizi sherehe zimetuleta pamoja na kutufanya kujisikia ni sehemu ya jamii lakini pia niseme Kwa sasa jamii imeshabadili fikra tofauti na ilivyokuwa kwa kipindi cha nyuma ambapo tulionekana hatuna mchango wowote kwenye jamii au taifa"anasema

















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI