Header Ads Widget

ACT WATOA MAPENDEKEZO KWA SERIKALI





*********************


Na Thabit Madai,Zanzibar -MATUKIO DAIMA


CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema Serikali ya awamu ya nane imo katika pirika za kukodisha huduma za ukodishwaji wa bandari kwa kampuni moja kutoka nje ya nchi.


Hayo yamelezwa na kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya sokoni Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Zitto amesema huduma za bandari na viwanja vya ndege ndio msingi wa uchumi wa Zanzibar kupitia sekta ya usafiri na uchukuzi na huduma hizo zinapaswa kusimmaia na serikali uendeshaji wake kutokana na umuhimu wake.

Akizungumzia ubinafsishwaji wa huduma za uwanja wa ndege wa Abeid AMani Karume Zanzibar na jengo la tatu la abiria katika uwanja huo, amesema serikali imebinafsisha kwa kapuni ya Dnata kutoka Dubai kinyume ya sheria ya ushindani na zabuni zilizopitishwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar.

Aidha amewataka wajumbe wa baraza la wawakilishi wa chama cha ACT Wazalendo kuhoji serikali imetumia vipi fedha za mikopo zilizotengwa kukopeshwa wajasiria mali kupitia benki ya CRDB zilizotolewa mkopo na shirika la fedha duniani IMF.

Mapema Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Othman Masoud Othman, amesema Sera ya Mamlaka Kamili ndiyo suluhisho pekee la kudumisha amani na utulivu wa wananchi, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Amesema kuwa pindipo Zanzibar ikirejesha Mamlaka yake Kamili, wananchi wote wataweza kuepukana na adha ya mateso, dhulma, kunyimwa haki, ubadhirifu na ukandamizaji.


Othman amefahamisha kuwa kukosekana kwa Mamlaka hayo mathalan, ndiko kunakopelekea jeuri ya baadhi ya maamuzi yakiwemo ya kupora maamuzi ya demokrasia ya wananchi na hata kuthubutu kufuta uchaguzi.

Hivyo amewataka wananchi wote kujenga mashirikiano katika kupigania kwa umoja Mamlaka Kamili ya Zanzibar ili kujenga amani ya kweli, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kwa upande wake mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Ismail Jussa Ladhu, amesema mikataba yote ya ukodishwaji rasilimali za umma itapitiwa upya na kufutwa baada ya chama cha ACT kushika madaraka ya nchi mwaka 2025.


Katika salamu zake, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Babu Juma Duni Haji, ameeleza azma ya Chama hicho, kuendelea bila ya kuchoka, kutetea Zanzibar Mpya, Yenye Umoja na Mamlaka yake Kamili, katika ngazi zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kabla ya Salamu hizo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, Bi Doroth Semu amewapongeza akinamama wa Zanzibar kuendelea kusimama imara katika kutetea demokrasia, ili liendelee kuwa fundisho kwa Taifa zima.


Viongozi mbali mbali wa Kitaifa wa Chama hicho wamehudhuria na kutoa salamu zao katika Mkutano huo wa Ufunguzi kwa hapa Visiwani, akiwemo Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Ado Shaibu Ado na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui; Katibu wa Uenezi na Mahusiano na Umma, Bw. Salim Bimani; Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho Bw. Omar Said Shaaban; Ismail Jussa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama; Bi. Pavu Abdallah Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake na Khadija Anwar Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Zanzibar.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI