Header Ads Widget

WAZAZI WALIOSHINDWA KUWAPELEKA WATOTO WAO KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA KUSAKWA NYUMBA KWA NYUMBA

  



NA, TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.


Mkuu wa mkoa wa kagera Albert Chalamila amewataka, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa shule kwa kushirikiana na madiwani kufanya msako maalumu wa nyumba kwa nyumba ili kuwabaini na kuwakamata wazazi na walezi ambao wameshindwa kuwapeleka watoto wao aliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.


Ameyasema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ili kuelezea hali ya uandikishaji wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ilivyo mkoani kagera ambapo amesekama kuwa, mpaka sasa ni asilimia 60 tu ndio waliokwisha kuripoti shuleni huku akisisitiza viongozi kupitisha msako mkali haraka iwezekanavyo  kila sehemu ili kuwabaini wazazi ambao wamekataa kuwapeleka watoto wao shule ili wachukuliwe hatua.


" Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika mkoa wetu walikuwa wanafunzi zaidi ya wanafunzi elfu 59, hawa wanafunzi ni wengi na tulitarajia kufika sasa wote watakuwa washajiandikisha shuleni na kuanza masomo kitu ambacho mpaka sasa kimekuwa tofauti, hivyo basi natoa amri wakuu wa wilaya zote mkoani kagera, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri kwa kushirikiana na walimu wakuu pampja na madiwani washirikiane kufanya misako kuanzia sasa ili tubaini wazazi ambao wamekuwa kikwazo cha kuwapeleka watoto wao shuleni kupata haki yao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao"


Aidha ameongeza kuwa, mzazi au mlezi yeyote atakayebainika amemtorosha mtoto ili asikamatwe atachukuliwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake huku akiwataka wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi kupokea ripoti kila siku kutoka kwa wakuu wa shule ili kubaini wapi kuna mkwamo patatuliwe haraka iwezekanavyo.


Sambamba na hilo, ametoa maelekezo kwa wakuu wa shule ambao wameshindwa kuwapokea wanafunzi kwa sababu ya kukoswa baadhi ya michango ya shule kuacha tabia hizo mara moja kwani atakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua kali ikiwemo kushushwa cheo.


"Natoa rai kwa walimu wakuu wa shule atakaye mkwaza mzazi kwa kuanzisha michango ambayo haipo kwenye utaratibu au  kugoma kumpokea  mwanafunzi kwa kisingizio cha kuwa ajakamilisha mchango fulani atachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kusimamishwa kazi au kushushwa cheo, tunataka watoto wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika mkoa huu wote wakajiunge na sio vinginevyo ili kuakikisha madarasa haya yaliyojengwa na mheshimiwa rais yanajaa"


Amesisitiza kuwa Kagera inabadilika endapo kila mzazi atampeleka mtoto wake akapate elimu kwa manufaa yake na jamii kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI