Header Ads Widget

VICTOR MAKUNDI "BILA CCM IMARA TANZANIA ITAYUMBA".



NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

MJUMBE wa Baraza kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Victor Makundi amesema bila kuwa na Chama cha Mapinduzi imara Tanzania itayumba.



Alisema kupitia safari za Rais Samia Suluhu Hasani na Diplomasia ya kiuchumi imesaidia nchi kufunguka katika uwekezaji.



Makundi alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na vijana wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Rombo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi ambapo zoezi hilo lilienda sambamba na upandaji miti katika shule za Sekondari Mamsera pamoja na Kelamfua.



Alisema kuwa, toka kuingia kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia uchumi wa Taifa umekuwa kwa kasi kubwa kutokana na kuwepo na wawekezaji wengi wanaokuja kuwekeza nchini.



"Kupitia safari za Rais Dkt Samia Suluhu Hasani na Diplomasia ya kiuchumi nchi yetu imefunguka milango kwa wawekezaji wengi kuja kuwekeza hapa nchini hali ambayo imepelekea uchumi wetu kukua kwa kasi kubwa" alisema Makundi.



Mjumbe huyo alisema kuwa, Serikali imejidhatiti kumaliza matatizo ya wananchi hivyo bila kuwa na Chama cha Mapinduzi imara Tanzania itayumba.



Alisema kuwa, Serikali imekuwa ikikopa kimkakati ili kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali na kuwataka vijana wa Chama cha Mapinduzi kuhakikisha wanaisemea miradi hiyo pamoja na kuilinda ili iweze kudumu.



Makundi alisema kuwa, Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu ya elimu hivyo jukumu la wanafunzi ni kusoma kwa bidii na kutumia nafasi hiyo kuwasihi wanafunzi kuwa na nidhamu ili kufanya vizuri katika masomo yao.


Kwa upande wake, Mwenyekiti UVCCM wilaya ya Rombo, Evance Mrema alisema kuwa, vijana wa Chama cha Mapinduzi wanajukumu kubwa la kuwa kijana wa mfano kwa kutekeleza mambo mazuri na ya kizalendo pamoja na kulinda Dola.



Mrema alisema kuwa, Uvccm wanajukumu kubwa la kukemea uovu na uahilifu katika jamii kwani kumekuwepo na unyanyasaji wa watoto hivyo wanawajibu wa kupambana na vitendo hivyo.


Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Kelamfua Agripina Laswai alisema kuwa, shule hiyo inakabiliwa na tatizo la ubovu wa miundombinu ya maji katika vyoo pamoja na uchakavu wa majengo.



Agripina alisema kuwa, pia shule hiyo inakabiliwa na mwamko mdogo wa jamii kuchangia chakula cha watoto mchana pamoja na ufinyu wa ruzuku inayotolewa na Serikali haitoshelezi mahitaji ya mitihani hasa mitihani ya vitendo.


"Motisha hafifu kwa walimu hasa wanaofanya vizuri katika masomo yao hivyo kushusha morali ya walimu kufanya kazi kwa bidii" alisema Agripina.



Katika maadhimisho hayo, Mjumbe huyo wa Baraza Victor Makundi alichangia laki tano kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji katika vyoo vya shule ya Sekondari Kelamfua.

Mwisho...


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI