Na Gift Mongi,MATUKIO DAIMA APP,Moshi
Naibu waziri wa utamaduni sanaa na michezo Pauline Gekul amezitaka halmashauri zote katika mkoa wa kKilimanjaro kuhakikisha zinatenga fedha kwaajili ya uendeshaji wa michezo ili kuhakikisha viwanja pamoja na vifaa vya michezo vinapatikana.
Aidha amezitaka serikali za mitaa kuhakikisha wanakuwa na maeneo kwa ajili ya michezo ili kukuza vipaji vya watoto pamoja na vijana pamoja na kuimarisha afya kupitia michezo.
Gekul ametoa agizo hilo katika bonanza la michezo lililoandaliwa na shirika la kuwezesha wanawake(Florida women empowerment) kushirikiana na umoja wa wanawake Tanzania wilaya ya Moshi Mjini lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha michezo nchini.
Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete ,kuvuta kamba,, kukimbia na magunia kufukuza kuku,kukimbia na yai kwenye kijiko, mdako, mchezo wa kuruka kamba huku washindi wakikabidhiwa zawadi mbalimbali na kusindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii wa mkoani hapa.
Waziri Gekul amesema ili kuendelea kuimarisha sekta ya michezo, viongozi kuanzia serikali za mitaa wanapaswa kuhakikisha wanatenga maeneo ya michezo, kuyalinda yasivamiwe na kuyaendeleza ili kuwasaidia wananchi na kukuza vipaji vya watoto pamoja vijana.
"Viongozi wa halmashauri mnapaswa kuhakikisha mnatenga fedha kwenye bajeti zenu kwaajili ya kuendesha michezo, suala la michezo ni la kila mmoja wetu, na jamii yote inapaswa kushiriki katika michezo, hakikisheni kwenye mitaa yenu mnakua na viwanja vya michezo, mnavitenga, mnavilinda na kama vipo hakikisheni mnaviendeleza" amesema Gekul na kuongeza
"Tunapoendesha michezo tujue tunajenga afya, mahusiano, undugu, tunaibua vipaji lakini pia tuajenga ajira, lakini kwa sasa hali ilivyo nchini kama sio kombe la mwenyekiti wa mtaa ni kombe la diwani au la mbunge, niwaombe viongozi wetu tengeni fedha kwaajili ya kuendesha michezo"amesema
Akizungumza katika bonanza hilo, Katibu wa chama cha mapinduzi wilaya ya moshi Mjini Ibrahimu Mjanaheri ameitaka serikali kuendelea kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji na makundi ya sanaa ili waweze kufikisha jumbe zao kwenye jamii.
"Tumeona kijana ameimba wimbo mzuri ambao wote umetuamsha hisia, na kutukumbusha umuhimu wa mama, kijana huyu anakipaji kizuri anachohitaji ni muda wa hewani kwenye vyombo vya habari ili aweze kutambulika,wapo wengine wenye uwezo wanachohitaji ni kuongezewa uwezo wa nyenzo pamoja na ujuzi "amesema Mjanaheri..
Kwa upande wake mwenyekiti wa UWT wilaya ya moshi mjini Theresia Komba amesema zipo programu mbalimbali za kimichezo zilizoandaliwa kwaajili ya wanawake na wasichana ambazo zimelenga kuwainua kiuchumi na kuwawezesha kukabiliana na aina yoyote ya dhuluma, manyanyaso, ukatili na ubaguzi.
0 Comments