ASKOFU wa kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa Dkt Blaston Gavile amesema kuwa mwaka ujao 2023 ni mwaka wenye dalili za mafaniko mengi ya mwilini na rohoni hivyo ataka angalizo kubwa kuwepo ikiwa ni pamoja na kuweka akiba ya mafanikio yatakayopatikana.
"Kama wachungaji naweka angalizo ,mwaka ukiwa na neema wengi tunajisahau na kuona ni haki yetu kupata mema bado nasisitiza tuweke akiba tutunze sisi kwa sisio tuombeane uzima kama familia"
Askofu Dkt Gavile aliyasema hayo juzi wakati akitoa salamu za Krismasi katika ibada iliyofanyika usharika wa Kanisa kuu Iringa , kuwa mbali ya mwaka ujao kuwa ni mwaka wa neema bado wananchi wanapaswa kutumia vizuri mvua za kwanza kuwa ni mvua ya kupandia mazao badala ya kuzitumia kuandaa mashamba .
Pia alitaka kila mmoja kuweka akiba ya chakula atakachokipata ili kuwa na akiba endelevu ya chakula kuwa iwapo akiba ya chakula itatunzwa vizuri si rahisi pale mvua zinapochelewa kunyesha watu kuwa na hofu ya njaa kwani tayari kila mmoja anakuwa na akiba yake mwenyewe ya chakula ndani .
Dkt Gavile alisema maandalizi mema ya familia yanapaswa kwenda sanjari na maandalizi mazuri ya kuwaandaa watoto vizuri kwa ajili ya shule kwani ili wasome vizuri yanahitajika maandalizi mazuri ya wazazi ili watoto wasikwame kwenda shule kutokana na sababu zozote zile .
Hata hivyo aliwataka watanzania kuendelea kuomba kwa ajili ya Taifa pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na watenda kazi wenzake ili nchi iendelee kuwa na amani na mshikamano .
Katika hatua nyingine askofu huyo ameitaka jamii hasa ya mkoa wa Iringa kuendelea kuomba na kukemea hali ya vitendo viovu vya ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo kwa sasa ndani ya mkoa huo vimeshika kasi hivyo lazima kuchukua tahadhali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo vuya ulinzi na usalama pindi vitendo hivyo vinapotokea katika maeneo yetu.
Aidha askofu Dkt Gavile alisema huu ni mwaka wa pekee ambao tunaadhimisha Krismas, tukiwa na baraka ya hali ya mvua, lakini tunasheherekea sikukuu hii mwaka huu bila KOVID 19 ni wema wa MUNGU tu, Mwaka 2022 umekuwa na mambo mengi sana yaliyo ya baraka, Mungu ametupitisha na kutuvusha katika mambo katika mambo mengi na ratiba nyingi, katika yote Mungu ametupigania, kuna wakati tumepita katika moto lakini hakutuacha tuangamie. Wapo kati yetu waliugua sana na kuuguza sana, hata hivyo wema wa Mungu umetuzunguka. Kweli hata sasa Bwana ametusaidia(Ebenezer).
Kwangu mwaka 2022 umekuwa ni mwaka wa kukumbuka sana hasa matukio mengi ya kanisa ndani ya Iringa na nje ya Dayosisi yetu ya Iringa, ikiwemo Mkutano wa wachungaji wote wa KKKT Tanzania nzima uliofanyika Dodoma, Mkutano wa wachungaji wa Dayosisi ya Iringauliofanyika Chuo Kikuu cha Iringa, Mkutano wa kurugenzi ya wanawake, malezi ya familia na watoto uliofanyika Arusha, Mkutano wa wachungaji watheolojia wanawake uliofanyika Njombe, uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi Kigoma, Mkutano wa LMC Mwanza, Mkutano Mkuu wa Dayosisi wenye wajumbe wapatao 700 ambao ulikuwa na uchaguzi wa saidizi wa askofu, na kwa pamoja Mkutano ulimchagua Mchungaji Askali Mgeyekwa kuwa Msaidizi wa Askofu kwa kipindi cha miaka 6 kuanzia 2022-2028. piamkutano uliwachagua wakuu wa majimbo na Idara.
Pia kumekuwa na zoezi la kuwaingiza kazini wakuu wa majimbo pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu, wakuu wa idara, vituo, vitengo na Taasisi, alisema Askofu Dkt Gavile.
Kwa upande wa usharika askofu Dkt Gavile amesema kuna ujenzi mkubwa wa makanisa ya kisasa unaendelea, nyumba za kisasa za watumishi, vitega uchumi mbalimbali vya sharika, sharika kumi mpya zitazaliwa 2023 na pia kuna ongezeko kubwa la wakristo.
Kwa kumalizia Askofu dkt gavile amesema mwaka 2022 ni mwaka ambao tulimwahidi Mungu kufanya mambo kadha wa kadha, mengine hata sasa hayajafanyika. Mwaka huu unapokwisha tumwungamie Mungu kwa mengi tuliyoshindwa na hata kutimiza wajibu wetu, Tumalize kwa toba, Lakini pia tuna mambo mengi tumemkosea Mungu. Kinachofurahisha Mungu ni moyo wa Toba, unyenyekevu na moyo wa Shukrani.
0 Comments