Na Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP,MOSHI.
Mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi leo desemba 12.2022 ameongozana na diwani wa kata ya Kimochi Ali Badi na afisa mtendaji wa kata Advela Mtangeki wameshiriki katika shughuli ya kuchimba na kujenga barabara itakayounganisha vijiji vya Mdawi, Shia na Kisaseni vilivyoko katika Kata ya Kimochi.
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa barabara hiyo itafungua shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijiji hivyo na kurahisha huduma za usafiri jambo ambalo limeonekana kuwa kero kwa muda mrefu .
Akiwa njiani kuelekea katika eneo inakojengwa barabara hiyo, Prof Ndakidemi almepata nafasi ya kupita katika kijiji cha Mdawi ambapo amejionea kazi ya awali ya ujenzi wa ofisi ya Kijiji kwa nguvu za wananchi ambapo bado wanaendelea kuchangia vifaa mbalimbali. Kwa kuunga mkono juhudi za wananchi ameahidi kuchangia matofali 800 katika mradi wa ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Mdawi.
Mbunge amehamasika kwenda Kimochi baada ya kubaini kwamba wananchi wa Vijiji vya Mdawi, Shia, Kisaseni vilivyoko katika Kata ya Kimochi wamehamua kutengeneza barabara ya kuunganisha vijiji hivyo kwa lengo la kurahisha huduma za usafiri kutoka na kuingia katika vijiji hivyo.
Wananchi hao wemeshaanza shughuli za kuchimba barabara hiyo kunakohusisha kupasua miamba na kukata miti mikubwa kwenye maeneo itakapopita barabara hiyo tarajiwa yenye urefu wa kilomita moja ambayo itakapokamilika itaunganisha vijiji hivyo vitatu.
Akiwa katika vijiji vya Kisaseni na Shia, Prof Ndakidemi allmewashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushirikiana kufanya kazi ya kuijenga barabara yao.
"Hapa nimejionea maajabu kwani akina mama ni wengi katika kazi hii ya kujitolea kuliko akina baba". Amesema mbunge.
Aidha ametoa wito kwa wadau wa maendeleo wa kata ya Kimochi wanaoishi nje ya kata wajitolee kusaidia kazi zilizoanzishwa na wanakijiji wenzao ya kutengeneza barabara na miradi mingine ya maendeleo.
" Niwaombe sana waunganishe nguvu kusaidia shughuli za maendeleo zinazoendelea katika Kata ya Kimochi maana maendeleo ni yetu site"amesema
Mwenyekiti wa Ujenzi wa Barabara hiyo Elisante Malima amemshukuru mbunge kwa kuwatembelea na kushiriki katika shughuli ya ujenzi wa barabara hiyo.
Amesema kwamba, uwepo wake umewatia moyo zaidi katika ujenzi wa barabara hiyo na pia wananchi wa vijiji husika wameamua kushirikiana kwa pamoja ili kujenga barabara ambayo itapitika msimu wote wa mwaka na itawasaidia kwenda zahanati ya Shia na pia kuwaongezea kipato kupitia shughuli zilizopo kwenye maeneo yao hasa zile za kilimo na ufugaji.
0 Comments