Katika kuelekea kipindi hiki cha mwisho wa mwaka jeshi la polisi mkoani Iringa limesema hali ya usalama mkoani humo ni shwari, hayo yamesemwa na kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Allain Bukumbi wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama kwa waandishi wa habari.
Kamanda Bukumbi amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata wanaojihusisha na vitendo vya kiuhalifu pamoja na mali za wizi kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Amesema Desemba 10, 2022 majira ya saa 10:00 jioni katika kijiji cha Kilangali Kata ya Image Tarafa ya Mazonmbe Wilaya ya Kilolo kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi walifanikiwa kumkamata Gwelino Mwanzasi mwenye umri wa miaka 91, mkulima wa Image ambaye alikutwa na silaha tano(05), silaha aina ya Gobore nne(04) na shortgun moja(1), Gololi za Gobore thelathini(30), risasi za Shortgun nne(04), risasi za G3 tatu(03), risasi za Riffle 375 moja(01), baruti ujazo wa nusu lita. jino la Kiboko moja(01), kipande cha ngozi ya Nyati kimoja (01) na gamba la Kakakuona moja(01), vitu hivyo vilikuwa vimefichwa katika chumba anacholala mtuhumiwa.
Aidha amesema katika operesheni zinazoendelea za jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Iringa wamelenga kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya kuwashambulia wananchi kwa kutumia mapanga na kuwapora mali zao ambapo mpaka sasa wanawashikilia watuhumiwa nane(08) na mapanga matano(05), vifaa vya kuvunjia pamoja na nondo.
Pia kamanda akaongeza kuwa katika mahojiano na watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na matukio mbalimbali ya kuvunja, kuiba na kushambulia watu kwa mapanga ambapo mali mbalimbali zimefanikiwa kukamatwa nazo ni runinga aina mbalimbali (13), Kompyuta mpakato(Laptop) mbili(02), Subwoofer tatu na Spika moja, pasi tatu na mashine ya kunyolea moja, magodoro matano ns kitanda kimoja, Ving'amuzi viwili na dish moja, Jiko la gas plate mbili na mtungi wa ORYX kg 30, mapanga manne, nondo moja, sare za ulinzi na toolbox ya vifaa vya kuvunjia.
Hali kadhalika Kamanda Bukumbi amesema wamemkamata Christina Mponzi, mwenye umri wa miaka 34, mkulima mkazi wa Kihesa akiwa na madawa yanoyodhaniwa kuwa ni Heroine kete 33, mtuhumiwa alikutwa akiwa ameweka kete hizo kwenye mkoba.
Na mnamo Desemba 18, 2022 saa 5:30 asubuhi katika kijiji cha Ifunda, Wilaya na Mkoa wa Iringa jeshi hilo kupitia askari wake waliokuwa kwenye msako waliwakamata watuhumiwa wawili Nassoro Mrisho na Consolatha Chonya wakiwa na kg 73 ya madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni bangi wakiwa kwenye chumba cha Consolatha Chonya upelelezi unaendelea na watuhumiwa bado wanashikiliwa na jeshi la polisi.
Na katika kuelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka kamanda Bukumbi amesema Jeshi hilo litaendelea kufanya operesheni ya nguvu zaidi ili kudhibiti uhalifu wa kijinai na ajali za barabarani. Pia ametoa wito kwa wakazi wotre wa mkoa wa Iribnga kujiepusha na vitendo vya kihalifu kuelekea sherehe za mwisho wa mwaka.






0 Comments