Na Gift Mongi, MATUKIO DAIMA,APP,MOSHI
Wazalishaji wa vyakula vya mifugo mkoani Kilimanjaro wamelazimika kupandisha bei za bidhaa hizo kwa kile kilichoelezwa ni uhaba wa malighafi ikiwemo mahindi ambayo kwa sasa yanauzwa kwa bei ghali ikilinganishwa na miezi michache iliyopita.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wafugaji hususan wa kuku wa nyama na mayai baadhi yao wamehamua kuachana na biashara hiyo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko faida wanayoipata.
Mkuu wa kitengo cha mauzo na masoko kutoka kampuni ya Marenga Millers ya mjini Moshi Deogratias Karoli amesema kwa kipindi cha muda mfupi kumekuwepo na mfumuko wa bei ya mahindi ambayo ndio rasilimali tegemezi katika kutengeneza vyakula hivyo.
Amesema kwa kipindi cha mwezi wa tatu na wa nne mwaka huu kilogramu moja ya mahindi ilikuwa ikiuzwa kati ya shilingi 700 hadi 800 lakini kwa sasa hali ni tofauti ambapo kilo moja ni kati ya 1200 na 1250.
Karoli anasema kuwa wakati wa mwanzoni mfuko mmoja wa kilogramu 50 wa chakula cha kuku uliuzwa kati ya elfu 50,000 hadi 56,000 ila kwa sasa kutokana na gharama kuongezeka bei imebadilika ambapo mfuko huo huo unauzwa kati ya 80,000 na 90000.
"Tunachokifanya hapa ni kama kutoa huduma sasa badala ya kufanya biashara maana kama mahindi hakuna ni dhahiri lazima vyakula vya mifugo bei iongezeke na sisi tukiongeza kama soko linavyohitaji wafugaji hawataweza kumudu gharama"anasema
Anasema kikwazo kilichopelekea kuadimika kwa mahindi hayo ni pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyopelekea mvua kutonyesha kwa wakati hivyo wakulima kukosa mavuno kama inavyokuwa kwa miaka mingine.
Pia sababu nyingine iliyotajwa na mkuu huyo wa kitengo ni kuruhusiwa kwa wakulima kuuza mahindi yao nje ya nchi hususan nchi jirani ya Kenya ambapo mahindi mengi yameuzwa huko huku viwanda vya ndani vikibaki bila kuwa na malighafi ya kujitosheleza.
Kwa upande wake Yunasi Swai ambaye ni meneja wa uzalishaji kutoka kampuni ya Joshi Diaries Ltd amesema wamelazimika kupandisha bei za vyakula vya mifugo kutokana na mahindi kupanda bei mara mbili ya walivyokuwa wakinunua hapo awali.
Amesema kutolewa kwa vibali vya kuuza mahindi nje na yenyewe ni changamoto kwani kumesababisha uhaba mkubwa jambo ambalo linaenda kutishia uhai wa viwanda vya ndani sambamba na wafugaji wenyewe.
Amesema changamoto nyingine mbali na mabadiliko ya tabia ya nchi ni pamoja na kupanda kwa mbolea katika baadhi ya maeneo ambapo wakulima wengi walishindwa kumudu bei hiyo hivyo kupelekea mavuno kuwa kidogo tofauti na uhalisia ulivyo.
"Naona ni muda sasa kwa serikali kutusaidia kuweza kupata mahindi kwa bei nafuu kama kutoka Zambia au Uganda ambapo kwa sasa ndio wanavuna ili tusije kufunga viwanda vyetu na wafugaji waendelee kufuga kama kawaida"anasema
Kwa upande wake naibu waziri wa wizara ya viwanda,biashara na uwekezaji Exaud Kigahe amesema kuwa kuadimika kwa mahindi kumetokana na wakulima kusafirisha nje kwa ajili ya kupata bei nzuri na kuwa kama kumesababisha uhaba wa malighafi hiyo serikali itaona njia nzuri katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Amesema kutokana na hali hiyo wazalishaji hao wanatakiwa kujipanga kuhakikisha wanakuwa na malighafi ya kutosha na kuwa wakulima nao hutafuta masoko ambayo ni mazuri kwa lengo la kujipatia faida.
"Hili tatizo kama serikali nilikuwa silijui ila nashukuru kwa taarifa na nitalifuatilia ili kuona njia nzuri za kuwasidia hawa wazalishaji wa vyakula vya mifugo"amesema
0 Comments