Shirika
la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) limeandaa msafara
wa siku 16 unaozunguka katika mikoa saba nchini Tanzania (Pwani, Morogoro, Singida,
Shinyanga, Geita, Mara na Arusha) kwa ajili ya kupaza sauti ya kupinga ukatili
wa kijinsia. Msafara huo ambao unahusisha wadau mbalimbali wa maendeleo na
viongozi wa Serikali umezinduliwa na Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima tarehe
25.11.2022 katika viwanja vya Leaders Club vilivyoko Kinondoni, Jijini Dar es
Salaam na utahitimishwa tarehe 10.12.2022 Jijini Arusha. Msafara huo unaongozwa
na kauli mbiu ya mwaka 2022 ya kupambana na ukatili wa kijinsia inayosema; “Kila
Uhai una thamani, tokomeza mauaji na ukatili
dhidi ya Wanawake na Watoto”. Mapambano haya sio mapya, kinachofanyika
Tanzania leo ni muendelezo wa kampeni ya kimataifa iliyoanzishwa na kituo cha kimataifa cha
wanawake katika uongozi (Women’s Global Leadership) mwaka 1991 kwa lengo la kukemea vitendo vya
ukatili wa kijinisia duniani kote ili kuifanya dunia iwe sehemu salama kwa
binadamu wote.
Mbali
na kujenga nguvu ya pamoja na kupaza sauti kukemea matendo ya ukatili wa
kijinsia nchini Tanzania msafara huu pia unalenga yafuatayo:
1. Kutoa
elimu kwa wananchi wa rika mbalimbali
wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari ili kujenga uelewa kuhusu ukatili wa jijinsia.
2. Kutambua
vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyojitokeza katika mkoa na maeneo husika.
3. Kutambua
mbinu wanazozitumia kukabiliana na vitendo hivyo katika maeneo yao.
4. Kutambua
changamoto wanazokubana nazo wakati wa mapambano ya ukatili wa kijinsia.
5. Kutambua
misaada wanayopatiwa wahanga wa ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
6. Kujadiliana
na kutoa mapendekezo ya mbinu bora zinazoweza kutumika kutokomeza ukatili wa
kijinsia.
Tayari
msafara umeshatembelea mikoa miwili, ambayo ni; Pwani na Morogoro na kupeleka
elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia. Katika Mkoa wa Pwani Msafara ulitembelea
wananchi wanaozunguka soko la Loliondo, Kibaha na Shule ya Msingi Tumbi. Mkoani
Morogoro Msafara ulifika na kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka soko la Chief
Kingalu na Shule ya Sekondari Mwembe Songo. Kwa ujumla, maeneo yote yaliyotembelewa, wananchi na
wanafunzi walisema kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia bado lipo kwa kiwango
kikubwa. Kwa mfano: vitendo vya ubakaji wa watoto, vipigo kwa wanawake na
watoto, ulawiti kwa watoto wa kike na kiume, matusi nk. vimekuwa vikiongezeka
siku hadi siku. Vitendo hivyi vimekuwa vikifanyika majumbani na shuleni na
vinafanywa na marafiki au ndugu wa karibu na hivyo watuhumiwa na wahanga
wamekuwa wakilindana na kukwepa mkono wa sharia kutokana na ukaribu walio nao.
Hii tabia ya kulindana imeleta changamoto katika harakati za mapambano ya
vitendo hivyi na hivyo kufanya tatizo liendelee kuwa sugu. Kwa maoni yao wananchi na wanafunzi wanapongeza
jitihada za Wizara na Shirika la WiLDAF pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa
jitihada hizi za kupinga ukatili wa kijinsia. Wanasema, Msafara huu wa kupinga
ukatili wa kijinsia umewafikia wakati muafaka ambapo wanahitaji jamii ilimishwe
ijue madhara ya vitendo hivyo na mbinu za kukabiliana navyo.
0 Comments