Adeladius Makwega-DODOMA
Mwanakwetu nilikuwa nimesahau
kabisa maana mara ya mwisho nilifanya kazi hiyo mwaka 2008 nikiwa mwanafunzi wa
shahada ya uzamili. Mtu na majirani zake, nikatoka hapo hadi kwa jirani,
nikaomba msaada huo kwa watu kadhaa, nikamkosa mtu mwenye ujuzi huo, nikiwa
nimekata tamaa nikakutana mama mmoja mgeni hapo nilipokuwapo, akanielekeza
vizuri sana na mimi kukumbuka hatua zote na kweli kazi yangu ilikamilika.
Mara baada ya kumaliza kazi
hiyo tu akaja ndugu mmoja akanisalimu, nikamuuliza vipi Songwe mmemchagua nani
kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo? Ndugu huyu akamtaja jina jamaa huyu na
kuitaja idara aliyokuwa akiifanyia kazi. Nikamuuliza Mkola mmemnyima? Ndugu huyu
akanijibu kuwa Mkola ni miongoni mwa majina kadhaa ambayo hayakurudishwa.
Kwa kuwa ndugu huyu ni
mwanaccm mzuri, namfahamu muda mrefu na ni kijana mkweli sana, japokuwa huo ukweli
wake huwa unamletea shida kidogo. Nikamuuliza je mna uhakika huyo Mwenyekiti
mpya wa CCM Mkoa wa Songwe anaweza kuhimili siasa za mkoa huo?
“Huyu jamaa anaweza,
tunamuamini na hata taasisi aliyokuwa anaifanyia kazi inatupa matumaini kuwa anaweza
kuifanya kazi hiyo.” Nikamuuliza ni hayo tu? Akasema ndiyo.
Nikamwambia kwani akichagulia
mtu kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, taasisi aliyekuwa anafanyia kazi anakwenda
kuitumikia tena au anakwenda kuwatumikia Wanaccm wa Mkoa wenu ? Akakaa kimya
ndugu huyu, nikasema kubwa akafanya kazi; kusimamia Katiba ya CCM, kusimamia maamuzi
ya vikao na kusimamia ilani ya chama hicho tawala cha siasa. Kazi yake
aliyokuwa anaifanya itabaki katika wasifu tu. Nikaagana na ndugu
yangu huyu na kuendelea na safari yangu.
Nikatoka nikafika eneo la pili
chumba kingine nikakutana na watu wengine wakawa wananitania, “Kaka naona leo
umevaa shati kubwa kubwa kama puto,” Nikasema ndiyo,mwingine akasema, “Kaka sijaona
bango lako katika mitandao ya kijamii vipi ujachukua fomu ya uongozi wa chama
chetu ?” Nikajibu Sijajaliwa kuchukua fomu hiyo.
Ndugu huyu wa pili akaniita
kando akasema nami kwa kunong’ona,
“Kaka mbona Dkt Bashiru Ally
anazingua? Wakati mama anaupigwa mwingi kweli kweli?”
Nikamjibu huyu ndugu yangu
nikisema kweli Dkt Bashiru Ally ana makosa, kwa leo ngoja nikwambie makosa mawili
tu. Ndugu yangu huyu akiwa amekaa katika kiti chake akaacha kuandika katika
kompyuta yake huku mimi nimesimama akawa ananisikiliza,
La kwanza kabisa Dkt. Bashiru
Ally hulka yake siyo mvivu kuongea, sasa kwanini alikaa kimya muda mrefu? Dkt.
Bashiru Ally ninayemfahamu mimi, akipigiwa simu na VOA, DW, BBC na vyombo
mbalimbali vya habari anaongea na kutoa maoni yake kwa kujiamini. Kama
hatoongea na wewe atakwambia,
“Nipigie simu baada ya saa
moja nipo nafundisha/ nipo kikaoni.”
Sasa imekuwaje akawa kimya kwa
muda mrefu? Katika hali zozote hulka yako usiipoteze. Kwa kukaa kimya alifanya
kosa kubwa na hapo tukawa na Dkt Bashiru Ally wawili; Mkimya wa sasa na
mwongeaji yule wa zamani.
Nikaendelea kumwambia ndugu
huyu huku akinitazama kwa umakini mkubwa, kosa la pili la Dkt Bashiru Ally
pahala alipoongelea hoja zake, huyo aliyemteua kampeleka Bungeni na anafahamu
fika kwamba huyu ndugu akienda huko ataongea hoja hizi nzito nzito na zilipaswa
kusikika Bungeni na Wabunge wengine tungeona maoni yao juu ya ndugu yao na
maoni yao yangenukuliwa katika karatasi za Bunge.
Ndugu yangu huyu akawa ananisikiliza
kwa makini mno, “Kabla ya ASP na TANU, wakati wa Sultani Jamshidi Bin Abdullah
na Gavana Edward Twining watu wa Zanzibar na Tanganyika walikuwa kwanza na
ajenda zao nyingi zilizokosoa utendaji wa serikali hizo , hizo ajenda ndizo
zilizozaa hivyo vyama na baadaye ndiyo ikazaliwa CCM.
ASP na TANU wazee wetu
walikutanishwa na ajenda, bila ya ajenda mpaka sasa tungekuwa chini ya tawala
zenye nasaba ya ndugu hao wawili yaani Sultani na Gavana. Viongozi wa sasa wa
CCM watake wasitakewa lazima watambue kuwa chama hiki ni mtoto wa AJENDA.
Alilolisema Dkt Bashiru Ally
ni juu ya wakulima wadogo wadogo akiwa na MVIWATA inayoongozwa Stephen Ruvuga.
Swali la kujiuliza je ajenda hiyo ya wakulima wadogo wadogo siyo ajenda ya
kudumu tangu ASP na TANU?
Cha kufanya siyo kumchukulia
hatua Dkt Bashiru Ally kwani ndugu huyu anatukumbusha ajenda ya wakulima wadogo
wadogo ambao ni mimi na wewe, ndiyo wenye CCM yao, ndiyo waliompigia makofi
Dkt. Bashiru Ally katika mkutano ule wa MVIWATA, hii ni ajenda ya chama chetu, kwa
kuwa ameshasema jukumu langu mimi na wewe tunapaswa kumkumbusha kuwa ndugu yetu
huyu amekaa kimya sana hadi tunadhani tuna Dkt Bashiru Ally wawili pia tunamuomba
hayo aliyoyasema MVIWATA akalonge pia katika vikao vya Bunge.
Mwanakwetu nikiwa nimevalia
shati langu kama puto nikakamilisha kilichonipeleka hapo nakurudi kwetu madongo
poromoka.
0717649257
0 Comments