Header Ads Widget

WALIOGHUSHI VYETI WATAKIWA KWENDA KWA WAAJIRI


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA Hosea Kashimba, amewataka watumishi wote waliondolewa kwa kosa la kughushi vyeti kwenda kwa waajiri wao ili kujaza fomu maalum kwa ajili ya malipo ya michango yao.


Pia, Mfuko huo unakadiria kulipa watu zaidi ya 9,000 na kiasi cha Sh. bilioni 20 kitatumika kama malipo ya fedha za michango walizozichangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii katika kipindi chao cha utumishi wa umma.


Kashimba, amesema maelekezo ya serikali yalitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, yalielekeza kuwa watu wote waliondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kughushi vyeti waanze kulipwa fedha za michango yao Novemba  Mosi mwaka huu.


“Rais ameelekeza watumishi hawa waliobainika kuwa na vyeti feki waanze kulipwa fedha zao za michango kuanzia Novemba mosi mwaka huu lakini kinachotakiwa hivi sasa kwa watu wote ambao walikutwa na sakata hili ni kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu ambazo zitaletwa kwetu kwa ajili ya malipo hayo.


“Badala ya kuja PSSSF, wanapaswa sasa kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu hizo na kuzilileta kwetu na sisi tutatoa kipaumbele kwao kwa kulipa ndani ya siku 60 tangu kuletwa kwa madai hayo”alisisitiza Kishimba


Aidha, amesema kabla ya kuunganishwa kwa mfuko huo mwaka 2018 walikuwa wanalipa pensheni kwa wastaafu Sh. bilioni 34 kwa mwezi.


“Baada ya kuunganishwa mifuko hii tumekuwa tukilipa pensheni kwa wastaafu Sh. bilioni 60 kwa mwezi na kila mwezi tunalipa wastaafu wapatao 150,000 na kila inapofika tarehe 25 ya kila mwezi tunahakikisha tumelipa”amesisitiza


Akizungumzia mchango wa uwekezaji wa mfuko katika uchumi amesema PSSSF ni mdau mkubwa katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi.


Amesema mfuko huo umewekeza Sh.trilioni 4.5 katika hatifungani za serikali.


“Pamoja na kuleta faida ya uwekezaji kwa mfuko kupitia riba na uwekezaji huu unauwezesha mfuko kutekeleza majukumu yake ya msingi. Vilevile mfuko umewekeza zaidi ya Sh.bilioni 500 katika soko la hisa la Dar es Saalam kupitia makampuni mbalimbali yaliyoorodheshwa”amesema


Kadhalika, amesema uwekezaji huo mkubwa wa mfuko unasaidia kukuza soko la mitaji nchini na kuchochea uchumi na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja.


Hata hivyo, amesema zaidi ya Sh.bilioni 400, zimewekezwa katika amana za muda (Fixed Deposit) katika benki mbalimbali nchini.


Msemaji Mkuu wa serikali Gerson Msigwa, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha kuwa wanafuatilia mara kwa mara waajiri wao kama wanawasilisha michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.


“Wafanyakazi ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa mnafuatilia kama waajiri wenu wanapeleka michango yenu katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kusiwe na shida pale ambapo mtumishi akifika wakati wa kustaafu”amesema Msigwa



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS