Moja ya vijiwe vya kahawa vilivyopo kijiji cha Kizenga Kigoma Vijijini
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Imeelezwa kuwa vilabu vya pombe na vijiwe vya kahawa vimekuwa vichocheo vikubwa vya vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wanaume kwa wanawake na watoto wakati mwingine kuvunja familia.
Hayo yameelezwa na wanawake wa vijiji vya Kalinzi na Kizenga halmashauri ya wilaya Kigoma wakati wa mikutano ya kampeni kuhamasisha jamii kupinga vita ukatili ambapo wamesema kuwa vijiwe hivyo ni tatizo kubwa kwao.
Akieleza kuhusu hali hiyo, Beatrice Karabona Mkazi wa kijiji cha Kalinzi alisema kuwa wanawake ndiyo wazalishaji mali kwenye mashamba na shughuli za biashara ndogo ndogo lakini waume zao wengi ni watu wa kukaa kwenye kupiga soga kwenye vijiwe vya kahawa, mipira na vilabu vya pombe.
Alisema kuwa kibaya zaidi wanaume wamekuwa wakichukua fedha zinazozalishwa na wanawake hao kwenda kutumia kwenye vijiwe hivyo na jambo hilo limesababishwa migogoro mingi ya kifamilia na familia nyingine kutengana.
Angela Jeremia Mkazi wa kijiji cha Kizenga Kigoma Vijijini akiunga mkono hali hiyo alisema kuwa vijiwe vya kahawa na vilabu vya pombe ni tatizo kubwa kwa familia na kwamba wakati mwingine wanaume wakirudi nyumbani wamelewa wanakuwa na manyanyaso na kuwapiga wake zao.
Alibainisha kuwa hali hiyo imesababisha kuvunjika kwa familia kwa wanawake ambao hawakubaliani na manyanyaso hayo na hivyo wanaume kuondoka na kususa kuhudumia familia zao.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya , George Vandesahuli alisema kuwa takwimu za kitaifa za masuala ya ukatili zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya matukio hayo yanatokea ndani ya familia kwa watu wa karibu kifamilia.
Vandesahuli alisema kuwa siyo jambo jema kuona kuwa familia badala ya kueneza amani na upendo ndiyo zinakuwa chanzo cha matatizo na mateso na kufanya familia kusambaratika hivyo wanawake na watoto kuwa wahanga wakubwa wa vitendo hivyo.
Afisa maendeleo ya jamii huyo alisema kuwa ni lazima jamii nzima iungane kwa pamoja katika kupinga vitendo vya ukatili kwenye familia ili kuzifanya familia kuishi pamoja kwa upendo na amani.
0 Comments