Serikali imezitaka
halmashauri na mabaraza ya miji Zanzibar kuhakikisha zinatumia fedha za Mfuko
wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa na
si vinginevyo.
Hayo yamesemwa na
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza
Hamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi Mhe. Hassan Sadiki Simai bungeni
Dodoma leo Novemba 08, 2022.
Mbunge huyo
alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kumaliza
malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa
Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar.
Mhe. Khamis
alisema Mfuko
huo upo kisheria namba 6 ya mwaka 2012 ambayo imeelekeza wazi kuwa fedha hizo zipitie
katika halmashauri na mabaraza ya miji.
“Mheshimiwa Naibu Spika sheria imeeleza wazi
kuwa fedha hizi zitakuwa zinapitia kwenye halmashauri na tulilifanya hili
kwasababu ilifika wakati tuligundua fedha nyingi zilikuwa zikitumika kinyume
cha utaratibu ndio maana Serikali iliamua sasa zilipitie kwenye halmashauri.
“Lengo la fedha hizi ni kuboresha miradi ya
maendeleo katika majimbo husika na si vinginevyo na pia fedha hizo zinapoingia
kwenye halmashauri husika wakurugenzi wawajulishe wabunge na pia wahakikishe
fedha hizi zinatolewa kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Khamis.
Awali akijibu
swali la msingi la mbunge huyo alisema Serikali imechukua jitihada za
kuhakikisha kuwa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zinawasilishwa
kwenye majimbo ya Zanzibar kwa wakati.
Alisema kuwa mtiririko
wa uwasilishwaji wa fedha hizo umekuwa wa kuridhisha, kwa mwaka 2022/23 ambapo sh.
bilioni 1,400,000 zimepelekwa Zanzibar Septemba, 2022.
Aidha, naibu
waziri huyo aliongeza kwa kusema kuwa katika mgawanyo huo wa fedha Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo za mwaka 2021/22 zilipelekwa Zanzibar Oktoba, 2021.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chaani Mhe. Juma Usonge Hamad
aliyehoji kuhusu kuchelewa kwa fedha za Mfuko huo kwa upande wa Tanzania
Zanzibar, Mhe. Khamis alisema changamoto zipo kwenye upande wa Serikali za
Mitaa.
0 Comments