NA THABIT MADAI, ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Dogo Iddi Mabrouk, amewataka, watendaji na wanachama wa jumuiya hiyo, kuondosha tofauti walizokuwa nazo kabla ya uchaguzi ili kuona jumuiya inaendelea kufanya kazi za chama sambamba na kuhakikisha CCM inaendeleza Ushindi wa Kishindo katika Chaguzi zote Nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Wakati wa Mapokezi Maalum yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Zanzibar ambapo alisema kuwa ili jumuiya iweze kuendelea kufanya kazi ni vyema ushirikiano uimarike ili kuweza kufanya kazi.
Alisema, uchaguzi umekwisha kilichobakia ni kuvunja Makundi na kuendelea kufanya kazi za Chama kwa Ushirikiano wa hali ya juu kama hapo awali.
"Mimi Sina budi nawashukuru sana wanachama wenzangu kwa kuniamini na kuniona nafaa kuongoza nafasi hii naahidi kukulipeni kwani mumenionesha imani na nitakulipeni Imani kwani nimeshinda kwa kishindo, Kilichobaki kuvunja Makundi na kufanya kazi za chama," alisema.
Hivyo, aliwataka viongozi na wanachama wa Jumuiya ya wazazi kumpa ushirikiano katika utendaji wake wa kazi ili kuona jumuiya hiyo inaendelea kwenda vizuri katika kufanya kazi zake.
Alishukuru Chama cha CCM kwa kumteua kugombea nafasi hiyo, na kuahidi kuendelea kufanya kazi nao kwa karibu na kuona wanashinda kupitia chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.
Sambamba na hayo, aliahidi kuwa jumuiya yao itakuwa ya mfano na kuendelea kushirikiana na chama ili kuona wanakivusha hasa katika chaguzi mbalimbali zitakazofanyika nchini.
Alisema, atahakikisha wanafikia Malengo katika Sera yao ya Elimu, Malezi na Mazingira.
Pamoja na hayo, alisema baada ya uchaguzi jumuiya imepanga mikakati ya kuona mipango yao kazi yanakwenda kama ilivyokuwa ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali ambayo yatatekelezwa chini ya viongozi waliochaguliwa hivi karibuni.
Sambamba na hayo, aliwataka wanachama hao kuacha majungu kwani hayasaidii katika utendaji wa kazi hasa za siasa kwani jumiya hiyo iweze kuwa mfano katika Chama.
Nae, Mwenyekiti wa jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mjini, Ali Othman Said, aliahidi kuendelea kumpa ushirikiano makamu wao ili kuona jumuiya hiyo inakwenda vizuri sambamba na kufuata miongozo na sera iliyokuwemo katika jumuiya hiyo.
Nao, wanachama wa jumuiya hiyo waliahidi kumpa ushirikiano ili kuona jumuiya hiyo inakwenda vizuri.
0 Comments