Wakati
askari wakilalamika kupunjwa mishahara na posho wanazostahili, Jeshi la Polisi
limeishukuru Serikali kwa jinsi inavyolijali kwa kuhakikisha posho na stahiki
nyingine zinalipwa kwa wakati.
Taarifa
iliyotolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime
ambaye ni msemaji wa jeshi hilo kutoka makao makuu jijini Dodoma, imesema licha
ya stahiki za askari wake, Serikali inalipa fedha za mafuta na vipuri vya
magari yanayopelekwa hadi kwa wakuu wa polisi wa wilaya ili kufanikisha
utendaji wao.
“Jeshi la Polisi linaishukuru Serikali ya awamu
ya sita kwa namna inavyolijali kwa mambo mbalimbali, kwani ni kipindi ambacho
kwa kiasi kikubwa tumeshuhudia posho na stahiki mbalimbali za askari
zikiendelea kulipwa kwa kasi kubwa kuhakikisha kila askari anapata posho
anayostahili,” alisema
Ingawa askari wenyewe wanasema utaratibu
umebadilika tangu Serikali izuie kukatwa fedha zao za posho ya chakula kila
wanapoenda kwenye mafunzo, Misime amesema Serikali imetoa Sh11 bilioni
kuwagharimia mafunzo yao na Sh11.7 bilioni kwa ajili ya sare za askari wote wa
jeshi hilo wanaozidi 40,000.
“Hayo yote yamefanywa na Serikali ili kuboresha
maslahi na vitendea kazi kwa askari polisi. Zipo taratibu za askari kuwasilisha
madai yake halali zinazofahamika kwa wote,” alitahadharisha Misime.
Katika jitihada za kuhakikisha askari wanafika
eneo la tukio kwa wakati, wanadhibiti uhalifu uliopangwa na kuwalinda raia na
mali zao kwa uhakika, Misime amesema Serikali imetoa Sh15 bilioni kwa ajili ya
kununua magari na tayari 80 yameshapokelewa na kusambazwa mikoani.
Magari mengine 72 amesema yanakamilisha
utaratibu wa usajili ili yasambazwe mikoani na vikosini, huku magari mengine
pamoja na pikipiki 336 kwa ajili ya doria yakiwa yameagizwa.
Kwa magari hayo na uwezeshaji
mwingine uliofanywa na Serikali kwa Jeshi la Polisi, Misime amesisitiza kwamba
“askari anayekwenda kwa raia na kudai ampe fedha ya mafuta ya gari, akibainika,
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake."
0 Comments