Header Ads Widget

DHANA YA UREJESHAJI WA UOTO WA ASILI INAVYOWEZA KUPUNGUZA UPOTEVU WA MISITU TANZANIA.



NA HADIJA OMARY, LINDI

......Takribani hekta milioni saba za misitu upotea Duniani kila mwaka huku jitihada za wadau mbali mbali zikifanyika ili  kupambana na changamoto hii kwa kuokoa uoto wa asili ambao unatajwa kuendelea kupotea kila uchwao  huku miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchagizwa kwa uharibifu huo ni pamoja na mabadiliko ya tabia ya Nchi, hali ya umasikini, ongezeko la watu, na kilimo cha kuhama hama.


Shirika la kimataifa la uhifadhi mazingira (WWF) linalofanyakazi na zaidi ya Nchi 10 barani Afrika ni miongoni mwa mashirika yanayopambana kuhakikisha wanarejesha uoto wa asili  kwa lengo la kuchangia hekta milioni 13 katika Bara lote la Afrika huku kwa Tanzania pekee likilenga kurejesha hekta milioni 2.6 kati ya hekta milioni 5.2 zilizopotea.


 
DKT, Lawrence Mbambo ni Meneja kutoka Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira (WWF) alisema   Shirika hilo limejiwekea mikakati na malengo tofauti katika Bara hilo la Afrika kufanya urejeshaji wa uoto wa asili (FOREST LANDSCAPE RESTORATION IN AFRICA)  ifikapo mwaka 2027.


Alisema katika malengo hayo Nchini  Cameroon imepanga kuchangia urejeshaji huo wa uoto wa asili kwa hekta milioni 3, DRC Kongo hekta 800,000, Zambia hekta 500,000, Uganda hekta milioni 1.25, Kenya hekta milioni 2.5 , Tanzania hekta milioni 2.6 na Zimbabwe kurejesha uhoto huo kwa hekta 250.000.

   

Nchini Tanzania Shirika hilo linafanya kazi katika kanda tatu ambazo ni kanda ya kusini (Ruvuma landscape) kanda ya maji mengi (water tawas ) pamoja na kanda mtambuka kati ya Kenya na Tanzania ambayo ipo kusini mwa kenya na kaskazini mwa Tanzania.


 Aidha Mbwambo alisema  katika kukabiliana na changamoto hiyo ya upotevu wa misitu WWF imekuwa ikishirikiana na wadau mbali mbali wa uhifadhi wa misitu ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wameanzisha dhana ya kufanya urejeshaji wa uoto wa Asili (FOREST LANDSCAPE RESTORATION IN AFRICA)  kwa kushirikisha Wadau wote ambao wanatumia Ardhi.


 “ sisi kama WWF tunajiunga na malengo ya Dunia kufikia mwaka 2030 la kurejesha uoto wa asili kwa takribani hekta milioni 350 ambapo Nchi za Afrika zikaungana na Nchi zingine Duniani kwa kuleta ahadi ya kurejesha uhoto wa asili kwa hekta milioni 100 katika mpango wa AFRI ONE HUNDRED ifikapo mwaka huo”.


 “Pamoja na jitihada zinazofanyika kuhakikisha tunarejesha uoto huo wa asili lakini bado hali ya uhalibifu wa misitu uongezeka mwaka hadi mwaka mathalani takwimu za mwaka 2017 zinazoonyesha hali ya Misitu Tanzania inaonyesha  jumla ya hekta laki  469,000 upotea kila mwaka” alisema Mbwambo.


 Kijiji cha Mchakama kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ni miongoni mwa vijiji  98 vinavyosaidiwa na Shirika la kuhifadhi mipingo na maendeleo MCDI kwa kushirikiana na Shirika la uhifadhi Mazingira WWF  ambavyo hufanya kazi ya kuvisaidia vijiji kutenga na kuhifadhi misitu yao ya Vijiji kwa lengo la Kurejesha uoto wa Asili .


 Ofisa kutoka shirika la kuhifadhi Mpingo  na Maendeleo MCDI, Joer Phares alisema ili kuendelea kuhifadhi msitu huo wa Kijiji cha Mchakama wenye ukubwa wa hekta 5,939 wamewawezesha wanajamii katika maswala kadhaa yanayowafanya kuondoa utegemezi wa kujipatia kipato kutoka kwenye msitu huo.


Akibainisha Zaidi alisema miongoni mwa mambo waliyowasaidia wanajamii wa Kijiji hiko cha Mchakama katika hifadhi hizo ni pamoja na  kutoa Elimu ya uhifadhi  Misitu inayolenga kurejesha uoto wa Asili kutoa misaada ya kuwezesha kazi kutekelezwa katika vijiji husika.


“mfano kama Kijiji hiki tumekiwezesha kutenga Msitu wa hifadhi wa Kijiji ambao unaheka Zaidi ya elfu tano na mia sita  na pia katika msitu ule tumewawezesha kufanya tathimini ya kujua raslimali zilizopo kwenye hifadhi ile na tukaweza kuwawezesha kutengeneza mpango wa uhifadhi na usimamizi wa msitu ukienda sambamba na mpango wa uvunaji” alisema Joel.


Kwa kipindi cha miaka 11  ambacho Kijiji hiko kimeacha utegemezi wa kufanya biashara ya mbao na miti kutoka katika msitu huo wa Hifadhi wa Kijiji MCDI imewawezesh wanajamii kupanda miti katika maeneo ambayo hayana miti (miti ya minungu nungu) pamoja na  kuanzisha kitalu cha miti  aina tofauti ikiwemo  miti ya asili iliyopo katika Kijiji hiko na miti ya mitiki  ambayo wanajamii wanaipanda katika mashamba yao ili kupunguza utegemezi wa matumizi ya miti ya asili .


 Bwana Phares aliendelea kueleza kuwa Kupitia Msitu huo wa hifadhi pia wamefanikiwa kuanzisha utalii ikolojia ambapo Kijiji kinakuwa kinanufaika kupitia  wageni wanaokwenda kutembelea kwenye vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi ambao  kwa kiasi kikubwa inapunguza pia utegemezi wa kufanya Biashara ya kuuza miti au mbao .


Ahamad ligambe ni katibu wa kamati ya Maliasili Kijiji cha Mchakama alisema wakati wanaendelea na jitihada za kurejesha uoto wa asili kwa kufanya uhifadhi wa Msitu katika Kijiji chao wanajamii  wameweza  kunufaika mambo mbali mbali  kutokana na faida wanazozipata kutokana na mauzo ya Magogo ya Miti yanayovunwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za uhifadhi

Ligambe anasema toka mwaka 2016 hadi 2022 msitu huo umekuwa ukiwapa faida wananchi kutokana na kuvuna magogo ya miti na kuyauza ambapo wameweza kukiingizia Kijiji kiasi cha Shilingi million 47.7 ambazo zimetumika katika  mambo mbali mbali katika Kijiji hiko.


Aidha Ligambe aliongeza kuwa Ili kuhakikisha msitu huo wa hifadhi wa Kijiji unazidi kuwapatia tija wamejiwekea utaratibu wa kufanya doria za mara kwa mara ikiwemo zile za kushtukiza ili kuweza kubaini endapo kunawavamizi wanao vamia msitu wao.


Hata hivyo alisema tokea Msitu huo wameanza kuuhifadhi kwa usimamizi wa shirika la Mpingo MCDI uvamizi katika msitu huo umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na Wananchi kutambua umuhimu wa msitu huo na faida wanazozipata kutokana na uhifadhi.

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya Kijiji hiko  Musa Musa alisema wanajivunia kwa uwepo wa Msitu wa hifadhi katika Kijiji chao kwani kupitia asilimia 50% ya mapato yaliyopatikana katika uvunaji wa magogo ya miti katika msitu huo wameweza kujenga ofisi mpya ya Kijiji, ununuzi wa nishati ya umeme jua unaotumika katika zahanati ya Kijiji , umaliziaji wa nyumba za walimu pamoja na kusaidia chakula cha Watoto Shuleni.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI