Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WANAFUNZI 405 wa shule ya Msingi Kumkambati iliyopo kijiji cha Mvugwe tarafa ya Makere wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wameshindwa kumaliza masomo yao ya elimu ya msingi kutokana na utoro sugu huku mimba na wengine kuolewa ikielezwa pia kuchangia changamoto hiyo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kumkambati, Ndabilole Raphael alisema hayo katika mahafali ya 19 ya shule hiyo na kusema kuwa ni wanafunzi 163 tu ndiyo walioandikishwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi katika shule hiyo kati ya wanafunzi 568 walioanza darasa la kwanza mwaka 2016
Mwalimu huyo Mkuu alisema kuwa katika wanafunzi hao wanaomaliza wanafunzi wasichana wapo 58 kati ya wanafunzi 266 walioanza darasa la kwanza mwaka 2016 huku wanafunzi wa kiume wakiwa 105 kati ya 302 walioanza darasa la kwanza.
Alisema kuwa sababu kubwa ya kushindwa kumaliza elimu ya msingi kwa wanafunzi hao ni utoro sugu unaochangiwa na wazazi wao wakulima kuhamia mashambani mbali ya maeneo hayo hivyo kuhama na watoto wao ambao pia wamekuwa wakitumika kwenye shughuli hizo za kilimo.
Pamoja na changamoto hiyo Mwalimu huyo alisema kuwa shule hiyo imekuwa na matokeo mazuri kitaaluma ambapo mwaka jana wanafunzi 88 waliofaulu walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kati ya wanafunzi 92 walioandikishwa kufanya mtihani huo.
Wakati Mwalimu Mkuu akieleza hayo baadhi ya wanafunzi walioongea na gazeti hili ambao majina yao yanahifadhiwa walisema kuwa wapo wanafunzi wenzao wengi wameacha shule wakiwemo wasichana ambao wamepata ujauzito na wengine kuolewa na wafugaji.
Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake Mwanafunzi wa shule hiyo,Cecilia Lucas alisema kuwa utoro sugu imekuwa changamoto kubwa shuleni hapo hivyo kufanya idadi kubwa ya wanafunzi wenzao kushindwa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.
Akizungumza katika mahafali hayo Meneja wa Shirika la World Vision Buhoma wilaya ya Kasulu, Donacian Severine amesema kuwa wazazi wanapaswa kubeba lawama kubwa ya utoro sugu wa wanafunzi hao kushindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Severine alisema kuwa wazazi ndiyo wenye wajibu wa kwanza wa kuhakikisha wanasimamia malengo ya elimu ya watoto wao na kwamba kushindwa kuhitimu masomo hayo siyo changamoto y wazazi pekee lakini pia ni changamoto ya taifa kuona litawatumia wapi watoto hao ambao kwa sasa hawajulikani wako wapi.








0 Comments