Na WMJJWM, Dar es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara hiyo itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria zinazosimamiwa na Wizara sehemu Wanajamii walipo kwa ajili ya kutatua changamoto zao.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo akifungua jengo la ofisi ya kikundi cha kijamii kinachoitwa Sauti ya Jamii katika Kata ya Kipunguni jijini Dar s salaam Oktoba 19, 2022.
Amesema vitendo vingi vya ukatili vinatokea kwenye jamii kwa asilimia kubwa ikiwa ni nyumbani hivyo Jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa nyumbani kunakuwa sehemu salama kwa watoto.
"Naambiwa kwamba taarifa zinaonesha kuna kushamiri wa ukatili, watu wanuana kwenye jamii, watoto wanakatiliwa kwenye jamii, wanaume pia, takwimu za mwaka 2021, watoto 11499 walikatiliwa, kati yao ni 5899 walibakwa, lakini asilimia 60 wamebakwa majumbani kwao na asilimia 40 mtaani" amesisitiza Mhe. Dkt. Gwajima
Mhe. Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba, hatakubali kuletewa taarifa ofisini, atakwenda kujionea mwenyewe yanayotekelezwa na wananchi kwani kuna maeneo mengine utekelezaji haupo au unasuasua hivyo ni jukumu la Wizara yake kufuatilia utekelezaji wa Sera mbalimbali katika ngazi mbalimbali nchini.
"Hatutaki kuletewa namba tukazikariri, bila kuwa tumeenda kushika, kama kuna changamoto tuzisikie, tuzijadili na tuwaeleze wanachotakiwa kufanya" amesisitiza Dkt. Gwajima.
Gwajima amezitaka kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zilizopo ngazi za kata, mitaa na vijiji kuiga mfano wa ubunifu wa kikundi cha Sauti ya Jamii kwa kuwa na shughuli zinazowaimarisha kiuchumi hivyo kutatua changamoto ya umaskini ambao ni chanzo kimojawapo cha vitendo vya ukatili.
Amesisitiza kutafuta na kuzitumia fursa mbalimbali zinazopatikana ili kujikwamua kiuchumi akibainisha mifuko 85 iliyopo kupitia Baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Awali akieleza kuhusu kikundi hicho mmoja wa wajumbe wa kikundi hicho Juma Rashid amesema waliamua wao wenyewe kuanzisha kikundi kwa lengo la kujiinua kiuchumi kupitia fedha zao wenyewe na hatimaye kujenga ofisi hiyo kwa gharama ya zaidi ya mil 11, yenye chumba cha mafunzo ya cherehani na ujasiriamali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipunguni Mhe. Steven Mushi ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuwawezesha wananchi hasa kwa kata ya Kupunguni ambapo jumla ya mikopo ya Halmashauri iliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2021/22 ni zaidi ya sh. Milioni 500.
"Kwenye Kata yetu hadi sasa tuna zaidi ya vikundi 50 na bado maombi ni mengi, tunashukuru pia kwa mfumo mpya wa kielekroniki utarahisisha kupata kwa wakati na kuondoa urasimu" amesema Mushi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wizalubi Ludigija amesema jitihada za Waziri Mhe. Gwajima za kuingia ndani ya jamii zimesaidia kufanya wanajamii kuifahamu Wizara na majukumu yake tofauti na hapo awali.
Amesisiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kutokomeza vitendo vya ukatili kwa maendeleo na ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.









0 Comments