Waziri wa Nishati,January Makamba, pamoja na Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic, Grace Olotu na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elisabeth Jacobsen wameshiriki katika warsha ya viongozi iliyofanyika kwenye mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia wa Equinor, Norway.
Warsha hiyo iliyowashirikisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,Kheri Mahimbali na uongozi wa juu wa kampuni ya Equinor, ilitoa nafasi kwa viongozi hao kujadili maandalizi ya mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG) Tanzania wenye thamani ya shilingi trilioni 70.
Waziri Makamba aliwahakikishia Equinor na washirika wake kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa majadiliano yote ya msingi kuhusu mradi wa LNG nchini yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.
0 Comments