Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wananchi wa mkoa Kigoma kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola ambao umeripotiwa nchi Uganda ili usiweze kuingia mkoani humo.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya wa afya ya msingi mkoa Kigoma alisema kuwa kwa sasa ugonjwa huo uko maeneo ya Mubende,Kasanga na Sagadi nchini Uganda umbali wa kilometa 800 kufika mkoani Kigoma lakini alisema kuwa umbali huo ni mfupi na upo uwezekano wa mgonjwa kutoka maeneo hayo akaingia mkoani humo na kuleta athari.
Akieleza hatua zilizochukuliwa Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk.Jesca Lebba alisema kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola yanadhibitwa kwa haraka iwapo atagundulika mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo kutokana na watoa huduma za afya mkoani humo kujipanga kikamilifu kutekeleza mpango wa kudhibiti ugonjwa huo.
Mganga huyo Mkuu wa mkoa Kigoma alisema kuwa mkoa umejipanga kila idara kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa bila kuleta madhara iwapo mgonjwa atagundulika mkoani humo.
Dk.Lebba alisema udhibiti huo umezingatia katika maeneo hatarishi ambayo yamekuwa na mwingiliano ikiwemo bandarini, kwenye vivuko vya mpaka na nchi jirani sambamba na viwanja vya ndege vya mkoa huo hasa kiwanja cha ndege cha Kigoma.
Alisema kuwa vipo vituo vya kupokea wagonjwa kwa kila wilaya, zipo gari zitakazotumika kwa ajili ya kusimamia taratibu za kuhudumia wagonjwa lakini pia uwepo wa watoa huduma waliopata mafunzo pamoja na vifaa vitakavyotumika pindi mgonjwa atakapopatikana.
0 Comments