Header Ads Widget

WALIOPISHA CHUMA CHA LIGANGA NA MAKAA YA MAWE LUDEWA NJOMBE KULIPWA FIDIA

 


Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE


Serikali Imeanza kufanya uhakiki wa mwisho ili kuanza zoezi la ulipaji wa fidia kwa wakazi wa wilaya ya Ludewa wanaotakiwa kupisha utekelezaji wa miradi wa chuma ya liganga na makaa ya mawe mchuchuma.


Mchakato huo umechukua takribani miaka saba  tangu kufanyika kwa uthaminishaji wa mali kwa watakaopisha mradi huo, ambapo baadhi  ya wakazi wa maeneo hayo hawaamini kama zoezi hilo linakwenda kufanyika hivi karibuni.


Baadhi ya wakazi hao akiwemo Costantine Mlowe,Brigita Stephani na Gerald  Steven  ambao ni wakazi wa Ludewa wanasema huenda sasa wakaanza kunufaika na miradi hiyo mikubwa.


Kwa sasa serikali imesema wananchi hao watalipwa fidia yao kulingana na uthamini uliofanyika pamoja na fidia ya kucheleweshwa kufanya shughuli zao za maendeleo ikiwa John Fute maarufu mzee Pwagu ambaye ni mbunifu wa zana za chuma anasema dhamira hiyo ni njema.


Zoezi hili limeanza kufanyika mara moja ili kuhakiki uhalisia wa wale wanaotarajia  kupisha utekelezaji wa mradi wa liganga na mchuchuma.



Dr. Yohana Mtoni ni  Mkurugenzi wa viwanda mama hapa nchini na Dr.Grace Aloyce yeye ni  mkurugenzi utafiti na mipango katika shirika la maendeleo NDC ambao wanatoa wito kwa wakazi wa Ludewa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uthaminishaji.


Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga wanasema kuelekea utekelezaji wa mradi huo wanufaika wa fidia wanapaswa  kuhakikisha wanafanya uwekezaji kwa kutumia fedha watakazolipwa ili ziweze kuwasaidia kuendesha familia.


Mradi huu unatizamiwa kuwanufaisha si tu wakazi wa Ludewa bali taifa zima kutokana na umuhimu wa rasilimali iliyojificha katika safu za milima hii. 


Madini ya chuma ambayo yanakadiriwa kuwa ni mamilioni ya tani zinazotarajiwa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka hamsini ijayo na kuzalisha mabilioni ya fedha za kigeni.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS