*********************
NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.
WALIMU wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Tumaini iliyoko kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba wamesema kuwa wanachangamoto ya uhaba wa walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu katika shule hiyo.
Changamoto hiyo imesemwa na mwalimu John Mwita anayefundisha katika shule hiyo kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili na usonji katika mahojiano maalumu na chombo hiki ambapo amesema kuwa nje na kuwa na miundombinu rafiki ya katika shule hiyo bado kuna changamoto ya uhaba wa walimu wanaofundisha kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu.
“Tuna jumla ya wanafunzi 74 wenye mahitaji maalumu katika shule yetu na sisi walimu tunaofundisha watoto wa aina hii tupo watatu, kiukweli hatujitoshelezi ukilinganisha na watoto tulionao kwani ukiangalia uwiano inatakiwa kuwa mwalimu moja kwa mwanafunzi mmoja hususa kwa watoto wenye usonji hivyo ukiwa na watoto sita wenye usonji utahitaji kuwa na walimu sita na sisi tupo watatu unaweza kuona jinsi tulivyo na uhitaji mkubwa wa walimu”
Aidha ameishukuru serikali kwa kuwawekea miundombinu ya kutosha ya madarasa huku akiiomba pia kuwapatia eneo maalumu la kujenga kiwanja cha michezo ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu walioko shuleni hapo kuweza kushiriki michezo itakayowasaidia kuchangamsha akili.
Kwa upande wake afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Bukoba, Maseke Sheja amesema kuwa serikali inaendelea kuajiri walimu nchini wakiwemo walimu wenye ujuzi wa kufundisha elimu maalumu ili kuweza kuondokana na changamoto hiyo.
“Walimu nikweli hawatoshi lakini sio katika shule wenye watoto wenye mahitaji maalumu tu bali hata katika shule nyingine lakini serikali inaendelea kuajiri walimu hata mwezi wa saba mwaka huu tumeona walimu wameajiriwa na wanaendelea kuajiriwa wengine hii yoye ni kuweza kutatua changamoto ya uhaba wa walimu wakiwemo wenye uwezo wa kufandisha watoto wenye mahitaji maalumu”
Aidha amewashauri walimu ambao wapo kazini wanaowiwa kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu kurudi chuoni kupata mafunzo ili wakirudi waweze kufundisha moja kwa moja katika shule zenye watoto wenye mahitaji maalumu kwani itakuwa njia moja wapo kutatua chanagamoto ya uhaba wa walimu katika shule hizo.
0 Comments