NA ARODIA PETER,MATUKIO DAIMA App
WATANZANIA hususan vijana wameshauriwa kutumia vizuri muda na simu zao za kisasa maarufu simu 'janja' kutafuta, kupata taarifa na maarifa mbalimbali yanayohusiana na ujasiriamali.
Vijana wameelezwa kuwa matumizi sahihi ya simu hizo yatawawezesha kujikwamua kiuchumi na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira zinazozikabili nchi nyingi duniani na Tanzania ikiwa ni mojawapo.
Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 13, 2022 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ubungo Plaza Limited, Andrew Kato wakati akitoa mada katika mkutano wa kujadili fursa za biashara Tanzania na utayari wa kwenda kidigitali lililoandaliwa na Taasisi ya Wahandisi wa Elektronikia na Umeme Tanzania (IEEE).
Kato ambaye pia ni Rais wa Chama cha Watalaam wa Miliki Ardhi na Nyumba Tanzania, amesema kuwa katika maendeleo ya teknolojia hakuna mtu ambaye anaweza kuachwa kando, hivyo ni muhimu kwa jamii wakiwamo vijana kutumia fursa hiyo kufanya biashara na kujiingizia kipato.
Alisema zaidi ya asilimia 50 ya watu kwa sasa wanatumia simu janja kufanya vitu mbalimbali, hivyo kama vijana na jamii nyingine ya Watanzania wanapaswa kuziangalia fursa za kidigitali zitakazowasaidia kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.
"Biashara sasa hivi imebadilika, mambo yapo kidigitali, hivyo watu wanapaswa kubadilika hasa namna wanavyotafuta wateja kuuza bidhaa zao kwakuwa walaji wao wengi wapo na taarifa nyingi kuhusiana na huduma tofauti," alisema Kato
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahandisi wa Eletronikia na Umeme (IEEE), Dk Dennis Mwighusa alisema katika mazingira ya aina yoyote yale suala la mabadiliko ya kiteknolojia na kidigitali hayaepukiki kwakuwa yanawezesha kurahisisha utendaji wa kazi na shughuli zingine za kila siku za watu.
Dk Mwighusa amesema kupitia Taasisi ya IEEE, kila wiki wamekuwa wakifanya kongamano lenye mada mbalimbali zenye lengo la kutoa elimu kwa jamii ambayo inaweza kuwasaidia katika shughuli zao mbalimbali za kila siku.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa IEEE, Dk.Zaipuna Yonah alisema bado elimu kubwa inahitajika kutolewa kwa jamii kuhusu namna ya kutumia simu za mkononi kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
"Ili kuweza kufanikiwa katika hilo watu wanapaswa kutambua kuwa kutembea kidigitali inawezekana kabisa, hivyo elimu ni lazima iendelee kutolewa kwa jamii ili iweze kujua jinsi maendeleo ya kidigitali yalivyo muhimu katika kujikwamua kiuchumi, " alisisitiza Dk Yonah.
1.Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahandisi wa Kieletroniki na Umeme (IEEE), Dk. Zaipuna Yonah, akizungumza wakati wa mkutano wa wahandisi wa kujadili fursa na ubunifu wa kiuchumi kupitia mifumo ya kidigitali, jijini Dar es Salaam
4. Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahandisi wa Kieletroniki na Umeme (IEEE) , Dk. Dennis Mwighusa wakati akijadili fursa na ubunifu wa kiuchumi kupitia mifumo ya kidigitali, jijini Dar es Salaam leo Oktoba 13, 2022.
0 Comments