Teddy Kilanga, Arusha
Serikali imeokoa fedha zaidi ya sh.trilioni 33.3 zilizokuwa nje ya urasimishaji na uendelezaji wa biashara hali iliyopelekea baadhi ya biashara kuwa na tija kwa wafanyabiashara.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo jumuishi cha urasimishaji na uendelezaji wa biashara katika halmashauri ya jiji la Arusha ,Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora,Jenista Mhagama mwaka 2004 serikali ilifanya utafiti na kubainisha upotevu wa fedha hali inayotokana na kutorasmishwa kwa biashara na ardhi kwa asilimia 98.
"Utafiti huo ulibaini katika ya biashara tulizonazo nchini na zinazomilikiwa na watanzania asilimia 98 hazikuwa biashara rasmi kutokana na kutosajiliwa na kutojulika zilipo na wale wanaofanya hizo biashara hakuna tija yoyote kwao,"alisema Waziri Mhagama.
Aliongeza kuwa asilimia 89 ya ardhi na hasa maeneo ya vijijini ilikuwa haijarasmishwa kwani watu wengi hawakuwa na hati ya umiliki hali iliyokuwa inapelekea kushindwa kukopesheka na vyote hivyo vilikuwa na thamani ya fedha zaidi ya sh.trilioni 30.
Waziri Mhagama alisema baada ya serikali kubaini changamoto hiyo waliamua kuanzisha vituo vya urasmishaji na uendelezaji biashara(Mkurabita) ili kuweza kuokoa upotevu wa fedha pamoja na kuongeza tija ya biashara wanazofanya wafanyabiashara katika kila halmashauri.
"Yaani tunakuwa na fedha ya kitanzania ya thamani hiyo lakini imekuwa haifanyiwi kazi ya uendelezaji ikiwa wenye mitaji hiyo ya rasilimali walikuwa hawaonji rasilimali biashara na ardhi kuwa ni fedha kwao hali hii ilileta msukumo wa serikali kuanzisha Mkurabita,"alisema Mhagama.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha,Hargeney Chitukulo alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 mkurabita ilifanya urasmishaji na uendelezaji biashara katika halmashauri ya jiji la Arusha na katika zoezi hilo waliweza kushirikiana na Taasisi mbalimbali ikiwemo Sido.
"Mkurabita kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Arusha pamoja na wadau mbalimbali imefanya urasmishaji wa biashara ndogo,kati katika kata tano ikiwa wafanyabiashara 1396 wamefikiwa na 840 wamepewa mafunzo ya kurasmisha na kuendeleza biashara zao,"alisema Chitukulo.
Naye Mtendaji mkuu wa Mkurabita,Dkt.Seraphia Mgembe amesema utekelezaji wa jengo hilo lilianza mwaka 2021 ikiwa hapo awali watekeleza utendaji kazi wao bila kuwa na kituo cha urasmishaji hali ambayo manufaa yake hayakuonekana kwa uhalisia.
Nao baadhi ya wafanyabiashara na watendaji wa serikali kupitia taasisi zake wamesema kituo hicho kimekuwa chachu ya kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kurasmisha biashara zao.
0 Comments