Na Scolastica Msewa, Kibaha
Naibu Waziri wa Uwekezaji Viwanda na biashara nchini Mheshimiwa Exaud Kigabe amewataka Watumishi wa Idara ya Ardhi Nyumba Maendeleo ya Makazi kutoa elimu kwa wananchi kwani wananchi wengi hawaelewi masuala ya upangaji wa matumizi ya ardhi.
Amesema hayo wakati alipopita katika banda la Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi lililopo Kibaha katika maonyesho ya tatu ya Uwekezaji na Biashara yanayoendelea katika viwanja vya maili moja standi kabla ya ufungaji wa maonyesho hayo yaliyofanyika kwa siku tano.
Alisema Watumishi hao waendelee kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha kuhusu upangaji wa matumizi ya ardhi ili wajue kama maeneo yao yamepimwa au hayajapimwa na yapo katika matumizi gani ili hata sekta binafsi wakija kwa ajili ya uwekezaji wasipate taabu.
Aidha akizungumzia urasimu wa kutatua migogoro ya ardhi Mheshimiwa Kigabe alisema utatuaji wa migogoro usichukue muda mrefu nakusababisha Mwekezaji anaamua kuamia sehemu nyingine na wengine kususa kabisa.
Mheshimiwa Kigabe alimuhoji Kamishina Msaidizi wa mkoa wa Pwani Hussein Iddi kwamba anatumia njia gani anatumia kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Pwani na kuwataka Watumishi hao kuwajibika kikamilifu kwa kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka na kwa haki pasipo kumwonea mtu yeyote.
Kamishina Msaidizi wa mkoa wa Pwani Hussein alisema tatizo lililopo ni kwamba wawekezaji wengi hupokelewa na mikono isiyo salama ya wauzaji wa ardhi na kujikuta wanaingia kwenye ardhi zenye migogoro kwa kununua ardhi kwa watu ambao sio wamiliki wa maeneo yao.
Alisema wanachofanya ni kutoa elimu ili kuitatua migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza mabaraza ya ardhi katika mkoa wa Pwani ambayo yanafanya kazi katika kata za mkoa huo kuwasaidia wananchi kutatua migogoro hiyo.
0 Comments