Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina Juni 30 2022 imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 852.98 sawa na asilimia 109.5 na kuvuka lengo la kutakiwa kukusanya shilingi bilioni 779.03 na asilimia 33.5 zaidi ya kiasi kilichokusanywa 30 June 2021 ambacho kilikuwa ni shilingi bilioni 638.87.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), Lightness Mauki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.
Lightness Mauki amesema kuwa Ufanisi huu umechangiwa na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya uwekezaji wa mitaji ya Umma, hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali katika kukuza mapato na kudhibiti matumizi pamoja na kuongezeka kwa shughuli za ufuatiliaji katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa chache zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na tunaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yetu ya msingi kwa umahiri ili ufanisi huu uwe endelevu,"Amesema Lightness Mauki
Ofisi ya Msajili wa Hazina ina wajibu wa kusimamia na kuhodhi uwekezaji wa mali zote za umma ikijumuisha Uwekezaji wa hisa katika Taasisi na Mashirika ya Umma na katika kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa au ina maslahi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Aidha, BLightness Mauki ameongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu la kusimamia shughuli zote za Taasisi, Wakala na Mashirika ya Umma nchini. Majukumu ya MWH yameainishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Msajili wa Hazina.
"Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa inasimamia Taasisi na Mashirika ya Umma 287. Kati ya hizi kuna Mashirika na Taasisi 237 ambayo umiliki wake ni zaidi ya asilimia 51 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257, Taasisi 40 zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache na Taasisi 10 za nje ya nchi. Thamani ya uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika hayo ni Shilingi Trilioni 70,"Amesema Lightness Mauki
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeanzishwa kupitia Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu), Sura 370,ikiwa na lengo la kusimamia uwekezaji na mali zingine za Serikali katika taasisi na mashirika ya umma, pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa au kuna maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 Comments