NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kwa kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa jimboni kwake.
Mbunge huyo alitembelea Kata ya Uru Mashariki na kuzungumza na viongozi wa chama cha Mapinduzi wa kata hiyo.
Akiongea na viongozi wa kata, Mbunge alielezwa kuwa kero kubwa zinazowasumbua ni pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama katika kata ya Uru Mashariki na ubovu wa barabara za ndani hasa zile za Mwasi Kusini - Mwasi Kaskazini - Mruwia hadi Materuni.
Kero nyingine ni ile ya Joint Venture na sintofahamu katika ushirika wa Uru East na Mruwia AMCOS.
Viongozi hao wa chama walimweleza ndoto yao ya kuona mifereji ya asili ikikarabatiwa ili iwapatie wananchi maji ya kumwagilia Kahawa na Migomba pamoja na swala la uchakavu mkubwa wa shule za Msingi Kishumundu na Mnini.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mbunge akiwa na viongozi wa Chama wa kata, alitembelea jengo la UWT ambalo limechakaa na linahitaji kukarabatiwa.
Viongozi hao walimweleza mbunge kuwa mtaalamu anaanda mchoro wa kuboresha jengo hilo na gharama zinazohitajika.
Mbunge akiongozana na Afisa Mtendaji wa Kata Kawiche, Diwani wa Kata hiyo Samwel Materu na diwani wa viti Maalumu, Delina Temba, walikagua ujenzi wa barabara ya Uru - Mamboleo - Materuni inayokarabatiwa kwa kiwango cha Lami na Moram.
Vilevile, walitembelea madaraja mabovu ya barabara za Kishumundu - Kyaseni, na ile ya Kishumundu - Mwasi Kaskazini ambayo yanaendelea kuporomoshwa na mmomonyoko wa udongo unaotokana na mvua.
Viongozi hawa kwa pamoja walikubaliana kusaidiana na kushirikiana kwenye ukarabati wa ofisi ya UWT pindi wakati utakapowadia.
Viongozi hao kwa pamoja walijadiliana na kukubaliana kubeba kero zilizojitokeza kama ile ya kukosekana kwa maji safi na salama na kuazimia kuziwasilisha MUWSA.
Kero za ubovu wa barabara na madaraja waliafikiana kuzipeleka TARURA, na ya uchakavu wa madarasa waliafiki madiwani wazipeleke Halmashauri.
Kuhusu swala la joint Venture na sintofahamu katika ushirika wa Uru East na Mruwia AMCOS, Mbunge aliahidi kulifikisha katika Kurugenzi ya Taifa ya Ushirika.
Mheshimiwa Mbunge aliwashauri viongozi wahusishe wadau mbalimbali na wananchi katika kujiletea maendeleo badala ya kuisubiri serikali ifanye kila jambo.
0 Comments