Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoani Kigoma inamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Yamungu Dunia kwa tuhuma wa wizi wa mashine 13 za boti wizi unaoelezwa ulitokea mkoani Rukwa.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa mwanzoni mwa wiki hii eneo la Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.
Akieleza mafanikio ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo Kamanda Makungu alisema kuwa inatokana na operesheni ya pamoja iliyofanywa baina ya polisi wa mkoa Kigoma na wenzao wa mkoa Rukwa katika mwambao wa ziwa Tanganyika kutokana na kuwepo kwa taarifa za matukio mfulizo wa mashine hizo zenye thamani ya shilingi milioni 41.
Moja kati ya Injini hizo 13 ilitambuliwa kuwa ni ya mtu mmoja anayefanya shughuli za uvuvi kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Rukwa na tukio hilo liliripotiwa kituo cha polisi Namanyere wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Baada ya mashine hiyo kutambuliwa kuwa ilikuwa ya wizi polisi waliweka mtego kujua mmiliki wa mashine hiyo na ndipo mtego wao uliowapeleka kumkamata mtuhumiwa ambaye kwenye upekuzi alikutwa na mashine nyingine 12 hivyo kufanya kuwa na mashine 13 ambazo umiliki wake hauna maelezo yanayojitosheleza,”Alisema Kamanda Makungu.
Aidha katika tukio lingine kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa polisi wakishirikiana askari wa hifadhi ya Taifa ya Gombe waliwakamata watu wawili wakiwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo nane vikiwa na thamani ya shilingi milioni 34.8.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika kijiji cha Murubona wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Bahati Sondese (54) Mkulima na mkazi wa kijiji cha Rungwe wilaya ya Kasulu na Hisea Samwel (42) mkulima na mkazi wa kijiji cha Kibande wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambapo watuhumiwa walihifadhi nyara hizo ndani ya begi wakiwa wanatafuta mteja.
0 Comments