Fadhili Abdallah, Matukio Daima APP-Kigoma
BARAZA la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji limewasimamisha kazi watumishi wa Manispaa hiyo kwa kushindwa kusimamia majukumu ya idara zao na kuisababisha halmashauri hiyo kuingia kwenye migogoro na wananchi.
Akitangaza uamuzi wa kusimamishwa kwa watumishi hao Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa hatua hiyo inakuja ikiwa ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kukabili migogoro mbalimbali ambayo watumishi hao wamekuwa sehemu ya chanzo cha migogoro hiyo na kufanya wananchi kuilalamikia halmashauri kuendesha shughuli zake bila weledi.
Waliosimamishwa ni pamoja na aliyekuwa Mkaguzi wa mji, Victor Julius ambaye imeamuliwa kurudishwa shuleni kufundisha, Kaimu Afisa Mipango Miji wa manispaa Steven Ambrose ambaye pia ni Mthamini wa halmashauri ambaye inaelzwa kushindwa kusimamia majukumu yake na kusababisha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi ambapo madiwani wamesema kuwa hawako tayari mtumishi huyo kufanya kazi tena kwenye halmashauri hiyo.
Wengine ni Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji,Ismail Sadiki ambaye anatuhumiwa kutoa vibali feki vya ujenzi,kutoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo ya wazi na kushindwa kusimamiwa kwa weredi majukumu yake hivyo kukuza migogoro ya ardhi kwenye manispaa hiyo
Aidha baraza hilo la madiwani limemsimamisha kazi pia Afisa Biashara wa Manispaa ya Kigoma Ujiji,Baraka Mfubusa kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji wa vyanzo vya mapato na hivyo kuikosesha halmashauri mapato.
Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa kusimamishwa kwa watumishi hao kumefuata taratibu zote ikiwemo tuhuma zao kuanzia kujadili kwenye kamati ya mipango miji,Ujenzi na mazingira ya halmahauri hiyo, kikao cha fedha na uongozi na tuhuma hizo kuwasilishwa kwenye kikao cha nidhamu na maadili ambacho mapendekezo ya vikao hivyo yaliwasilishwa na kupewa Baraka na baraza la madiwani.
0 Comments