NA, TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera
MKUU wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila wamewaomba viongozi wa dini katika mkoa huo kuwaombea viongozi wa kisiasa walioshika nyadhifa mbalimbali za kiutawala mkoani humo waweze kuyakumbuka mambo waliyoyaahidi kwa wananchi wao.
Ameyasema hayo wakati akiongea na viongozi wa dini mbalimbali pamoja na kimila katika kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa uliopo katika Manispaa ya Bukoba kilichokuwa na lengo kujadili mambo mbalimbali ya kimaendelo pamojana kuuombea mkoa huo, huku akisema kuwa viongozi wa dini wanao mchango mkubwa katika taifa hasa katika kudumisha amani.
“Nilikuwa napitia mafaili hela ziliwahi kuja hapa kwaajili ya kutengeneza mazingira ya stendi na soko lakini wanasiasa wa hapa wakaanza kuipasua Kagera kwa kuvutana kuwa hiki kiende huku na hiki kiende kule mwishowe fedha zikarudi zilikotoka, viongozi wa dini ombeeni viongozi wa kisiasa ili anapoingia madarakani wawe na moyo wa dhati wa kusaidia wananchi wao yale waliyowaahidi kuwasaidia” alisema RC Chalamila.
Amesisitiza kuwa mkoa huo unawahitaji watu wenye maono mrefu wala sio ya muda mfupi huku akiwataka viongozi wenye maono ya muda mfupi wazuiliwe kwa maombi.
Ameongeza kuwa, viongozi wa dini wanayo nguvu ya kuyaona mambo ambayo kwa wakati mwingine viongozi hawayaoni hivyo wasisite kuyakemea huku akiwasihi kuhubiri amani kwa nguvu zote na kukemea vitendo viovu ikiwemo kuoneana wivu.
Kwa upande wake Shekhe wa mkoa wa Kagera Kharuna Kichwabuta akitoa neno kwa niaba ya viongozi wa dini amesema kuwa, viongozi wa dini wako bega kwa bega naviongozi wa serikali ili kuhakikisha mkoa wa kagera unapata maendeleo huku akimuomba mkuu wa mkoa huo kupambana kupunguza vizingiti barabarani ambavyo vinaonekana kuwa kero katika mkoa wa Kagera.
“Tunakushukuru mkuu wa mkoa kwa maono uliyokuja nayo ya kuuinua mkoa huu katika janga la umasikini lakini pia katika kupambana na janga hili nikuombe pia upambane kuondoa na vizingiti barabarani vimekuwa kikwazo kwa wananchi pamoja na wafanya biashara, leo hii kutoka hapa mpaka Mutukula unakutana na vizingiti kibao hii inatusumbua sana” Alisema Shekhe Kichwabuta.
Amemuomba pia mkuu wa mkoa huyo, kuwashauri viongozi wengine kuwa na mapokeo mazuri ya wawekezaji wanapokuja katika maofisi zao wakitaka kuwekeza na kuondoa vizingiti vya kuwazungusha huku akisisitiza kuwa wawekezaji wamekuwa wakifika katika maofisi kwaajili ya kuwasilisha maombi ya uwekezaji ila mapokezi ya watumishi hao sio mazuri suala lilipelekea wengine kwenda kuwekeza katika mikoa mingine ambapo watapata mapokezi mazuri.
0 Comments