Mwanariadha wa mbio fupi kwa wanawake Winfrida Makenji mchana huu ameondolewa mashindanoni baada ya kukutwa na kosa katika kuanza mbio za mita 100 katika Uwanja wa michezo wa Alexander jijini Birmingham, Uingereza.
Winfirida, mwenye umri wa miaka 21, ameelezwa na kocha wake Suleiman Nyambui kwamba ni mkimbiaji hodar ila hofu ya mashindano pamoja na kukosa uzoefu wa kushindana mara kwa mara vimechangia kuondolewa kwake mwanzo tu wa kuanza mbio.
Nyambui amesema Winfrida alifanya kosa la kuchomoka kabla ya mlio wa bastola ya kuanzia kulia, ambapo katika mashindano makubwa kama haya adhabu yake ni kutolewa (disqualified).
Winfrida amebakiza mchuano wa mbio za mita 200 ambao atashindana siku ya Alhamisi Agosti 4, 2022, ambapo atakimbia raundi ya kwanza. Akipita ataingia raundi ya pili siku ya pili Agosti 5.
Siku hiyo hiyo ya Agosti 4 mwanariadha Andrew Boniface Rhobi ataingia uwanjani kuchuana katika mbio za mita 1,500.
Rhobi, ambaye ana umri wa miaka 32 atajiunga na wanariadha wengine wa nchi mbalimbali kujaribu kuvunja rekodi ya mbio hizo za mita 1500 inayoshikiliwa na Mtanzania mwingine Filbert Bayi kwa miaka 48 sasa!
Leo Agosti 2, 2022 usiku mwanariadha Joseph Tiophil Panga ataingia uwanja wa michezo wa Alexander kuchuana katika mbio za mita 10,000
Wanaradha wawili wa kiume waliobaki watakimbia Agost 6, 2022. Nao ni Josephat Joshua Gisemo na Faraja Lazaro Damas wote watashindana katika mbio za mita 5,000
WAKATI HUO HUO NGUMI KUENDELEZA USHINDI Leo usiku bondia wa tatu wa Tanzania Kassim Mbundwike ataingia ulingoni kuipeperusha tena bendera ya Tanzania leo kwenye masumbwi dhidi ya Rafail Pafios kutoka Cyprus katika mzunguko wa 16 bora uzani wa Light middleweight 67kg - 71kg.
Pambano hilo bout no. 100 litaanza majira ya Uingereza saa 2.30 usiku (Tanzania saa 4.30 usiku) mshindi ataingia hatua ya robo fainali katika uzani huo.
MUNGU IBARIKI TANZANIA






0 Comments