NA WILLIUM PAUL, SAME.
WANANCHI wa kitongoji cha Nadururu kata ya Maore wilayani Same mkoani Kilimanjaro waliokuwa wakishinikiza kutohesabiwa katika zoezi la Sensa Agosti 23 mwaka huu kutokana na mwenzao kuuwawa na Tembo hatimaye wamekubali kuhesabiwa.
Hatua hiyo ya kukubali kuhesabiwa imekuja mara baada ya Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya kufika katika kitongoji hicho na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi hao na kueleza hatua mbalimbali ambazo serikali inazichukua katika kupambana na Tembo wanaofika katika makazi ya watu.
Mpogolo alisema kuwa, kutokana na kitongoji hicho kupakana na hifadhi ya Mkomazi na hali ya ukame iliyopo katika hifadhi Wanyama mbalimbali wakiwamo Tembo wamekuwa wakitoka na kuingia katika makazi ya watu kutafuta maji.
“Nimekuja hapa tujadiliane kwa pamoja nini tufanye maana serikali inataka hifadhi ya Mkomazi ibaki hapo ilipo na Kitongoji cha Naduduru nacho kibaki kama kilipo lakini kusiwe na mauaji ya wananchi yanayotokana na mnyama Tembo sasa nimekuja tushauriane kwa pamoja tufanye nini” alisema Mpogolo.
Akitoa maagizo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, shule haiwezi kufungwa kwa kuhofia Watoto kukutana na Tembo na kupata madhara na badala yake aliagiza Watoto kutowahi asubuhi kwenda shule bali wafike saa mbili asubuhi na wawe wanatembea makundi ambapo watakuwa wakisindikizwa na mtu mkubwa.
Mpogolo aliwataka Tawa na Tanapa kuendea kuboresha miundombinu ya hifadhini kwa kuchimba visima vitakavyokuwa vikitoa maji ambapo yatajazwa katika mabwawa yaliyopo ndani ya hifadhi hali ambayo itapelekea Wanyama hao kutotoka nje kutafuta maji.
Pia aliwaagiza Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA), kuwa na kempu katika kitongoji hicho cha Nadururu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na Tembo.
Kuhusu swala la barabara, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuonyesha sehemu ambapo itapita barabara ya kuingia katika kitongoji hicho kwa kufeka ambapo na yeye atawaagiza Tarura kufika kutengeneza barabara hiyo.
Akizungumzia swala la Sensa Agosti 23 mwaka huu, Mpogolo alisema kuwa, zoezi hilo ni muhimu kwa wananchi wote kujiletea maendeleo kwani Serikali inaleta miradi mbalimbali ya maendeleo kulingana na idadi ya watu.
“Wananchi wa kitongoji cha Nadururu kama mnania ya dhati ya kupata maendeleo ni lazima mhesabiwe hii itarahisisha Serikali kujua kitongoji hiki kinawatu wangapi na hata Mbunge na Diwani wenu watakuwa na nguvu ya kuwapigania na kuwasemea matatizo yenu kama ili la mwananchi kuuwawa na Tembo ili serikali iwasaidia” alisema Mpogolo.
Kuhusu swala la njaa kutokana na mazao yao kuharibiwa na Tembo, Mpogolo alisema kuwa kwa sasa serikali inaendelea kufanya tathimini ya kujua vijiji na vitongoji vingapi vipo katika hali mbaya ili waweze kupatiwa chakula kwa gharama nafuu na kuwataka kuendelea kuwa wavumilivu.
Awali Muikolojia wa Ikolojia ya Ruvu-Same-Kalemawe na mto Umba kutoka Tawa, Johson Bernad alisema kuwa, swala la Tembo ni changamoto ya kitaifa ambapo wilaya 54 zinakabiliwa na tatizo hilo.
Bernad alisema kuwa, awali serikali ilichimba mabwawa ndani ya hifadhi za Wanyama ili kuhakikisha wanapata maji ya uhakika lakini kutokana na hali ya ukame mabwawa hayo yamekauka na kupelekea Wanyama mbalimbali kama Tembo kutoka hifadhini kwenda katika makazi ya watu kutafuta maji.
Alisea kuwa, kwa sasa Serikali inajenga vituo maalum ambapo huwekwa wataalam kwa ajili ya kufukuza tembo pindi wanapoingia katika makazi ya watu kabla hawajaleta madhari kwa wananchi lakini pia wapo katika mpango wa kuwafunga kola Tembo kiongozi wa kundi itakayokuwa ikionyesha mahali watakapokuwa Wanyama hao.
Aidha aliongeza kuwa, kwa sasa wanaendelea na mpango wa uchimbaji wa visima vya ardhini ndani ya hifadhi ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika katika mabwawa yaliyopo ndani ya hifadhi.
Naye Mkuu wa Idara ya ulinzi hifadhi ya Mkomazi, Ezrome Lema alisema kuwa, kwa sasa hifadhi ya Mkomazi ipo katika mpango wa kutoa mradi mkubwa wa maji kuto Kisiwani hadi ndani ya hifadhi pamoja na mradi mwingine kutoka Lushoto mkoani Tanga lengo ni kuhakikisha maji hayakosekana ndani ya hifadhi.
Lema alisema kuwa, miradi hiyo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na wameshaomba fedha Serikali na kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupunguza kwa Wanyama kufika katika makazi ya watu kwani watakuwa wakipata maji ndani ya hifadhi.
Kuhusu swala la elimu ya kujikinga na Wanyama, Lema alisema kuwa wamekuwa wakifanya hivyo na kutoa rai kwa wananchi wa Kitongoji hicho cha Nadururu pindi watakapofika wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata elimu hiyo.
Mwisho….
0 Comments