MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Edward Mpogolo amesema kuwa wilaya hiyo imejipanga vya kutosha kuhakikisha wananchi wote wanahesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23 mwaka huu.
Mpogolo alitoa kauli hiyo wakati wa shindano la bonanza la mpira wa miguu lililoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki Anne Kilango Malecela na kufanyika katika viwanja vya Turiani kata ya Ndungu likishirikisha timu nane lenye lengo la kuhamasisha Sensa.
Alisema kuwa, mpaka sasa makarani pamoja na wasimamizi wa sensa wameshapatiwa mafunzo ambapo watasambazwa katika maeneo mbalimbali na kuwataka wananchi kuwapa ushirikiano na kujibu maswali watakayoulizwa kwa usahihi.
"Sisi kama Serikali ya wilaya tumeshakamilisha maandalizi yote muhimu ili kuhakikisha zoezi hili linaenda kwa usahihi mkubwa hivyo niwaombe wananchi mtoe ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa sahihi na msiwafiche ndani watoto wenye ulemavu pamoja na wazee kwani nao wanahaki ya kuhesabiwa" alisema Mpogolo.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Same mashariki Anne Kilango Malecela kwa kufanya mambo makubwa katika Jimbo lake na kuwatetea wananchi waweze kupata maendeleo.
"Nimetembea majimbo mengi lakini sijawahi kuona Mbunge mchapakazi kama Anne Kilango Malecela amefanya makubwa kwa kila rika hivyo niwaombe
wananchi muungeni mkono Mbunge wenu anawapambania sana" alisema Mpogolo.
wananchi muungeni mkono Mbunge wenu anawapambania sana" alisema Mpogolo.
Aliongeza kuwa Jimbo la Same mashariki ni wakulima wazuri ambao huitaji pembejeo za kilimo kama mbolea hivyo majibu yao yatapatikana kwa kushiriki kwa ukamilifu zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Naye Mbunge Anne Kilango Malecela alisema kuwa, bonanza hilo ni maalum kwa ajili ya uhamasishaji wa sensa na kuwataka wananchi kushiriki zoezi hilo Agosti 23 mwaka huu kwa ukamilifu na kutoa majibu sahihi katika madodoso.
Anne Kilango alisema kuwa, lengo la Sensa ni ili Serikali iweze kutambua idadi ya wananchi wake pamoja na kugawa maendeleo kulingana na idadi ya wananchi.
"Mkijitokeza kwa wingi kuhesabiwa mtanifanya mimi Mbunge wenu kupata fedha nyingi katika mfuko wangu wa Jimbo ambapo fedha hizo zinatumika kutatua changamoto zinazowakabili lakini tukijitokeza wachache ndivyo fedha zinavyopungua hakikishine hiyo tarehe hakuna mwananchi wa Jimbo letu analala nje na Jimbo" alisema Anne Kilango.
Katika bonanza hilo lililoshirikisha timu za Sulerstar, Kihurio rangers, Maore fc, Majengo fc, Aston villa, Mkonapa fc, Newcastle fc na Nyuki fc.
Timu ya Superstar iliibuka mshindi na kujinyakulia laki tano huku mshindi wa pili Maore fc akijinyakulia laki tatu na mshindi wa tatu Nyuki fc akijinyakulia laki mbili.
Mwisho..
0 Comments