NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
SERIKALI imejipanga kununua miche bora na ya kisasa milioni 20 na kuigawa bure kwa wananchi pamoja na kutenga milioni 150 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi alipafanaya ziara katika kata ya Kibosho Magharibi ikiwa na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Prof. Ndakidemi alisema kuwa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2022/23 Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imetenga fedha nyingi kwa ajili ya sekta mbalimbali.
Aliwaomba wananchi wa kata ya Kibosho Magharibi kuchangamkia fursa hiyo kwani kata hiyo ni maarufu kwa uzalishaji wa zai la kahawa hasa vijiji vya Manushi na kuwataka kuchangamkia miche hiyo chotara itakayotolewa na Serikali.
"Katika Bajeti ya 2022/2023 Serikali imetenga fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo yapo mambo mengine mazuri kwenye bajeti ya mwaka huu ni uwepo wa ruzuku kwenye miche ya kahawa, miparachichi na Mbolea tuchangamkie hii fursa" alisema Prof . Ndakidemi.
Katika ziara hiyo Mbunge alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo aliambatana na watendaji wa serikali wa kata, Kamati ya siasa ya Kibosho Magharibi na mwakilishi wa TANESCO.
Prof. Ndakidemi alitembekea na kukagua ujenzi wa nyumba ya kuishi ya Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Manushi pamoja ujenzi wa jengo la choo katika shule za msingi Manushi Chini na Wereni.
Vyoo hivyo vimejengwa kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo, wananchi, Halmashauri ya Moshi ambapo choo cha shule ya Msingi Manushi Chini kilipata kiasi cha shilingi milioni 3 kutoka kwenye mfuko wa jimbo.
Akiwa katika maeneo hayo, mbunge alielezwa kuwa kuna changamoto ya fedha za kukamilisha miradi hiyo na Mbunge alimwelekeza Diwani washirikiane ili wawasilishe tatizo la uhaba wa fedha za kumalizia miradi hiyo kwa wadau wa maendeleo na Halmashauri ya Moshi.
Aidha Mbunge huyo alishiriki katika mkutano wa hadhara katika vijiji vya Manushi mashariki, Wereni na Umbwe Onana kwa nyakati tofauti.
Akiwa katika kijiji cha Manushi Mashariki, Mbunge alikagua mradi wa ujenzi wa ofisi ya kijiji inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo aliwaunga mkono wananchi kwa kuchangia shilingi laki tano.
Akimkaribisha mbunge kuongea na wananchi, Diwani wa Kata hiyo Prosper Emil Massawe alimpongeza Mbunge kwa kuwa karibu nao wakati wote wanapomuhitaji na kuwasaidia kutatua changamoto za kata hiyo.
Massawe aliwaambia wananchi kuwa kata ya Kibosho Magharibi ni miongoni mwa kata zilizofaidika na miradi mikubwa ya maendeleo kama ile ya Ujenzi wa barabara inayotoka kwa Rafael kwenda Kombo ambapo madaraja ya kisasa yamejengwa.
Mradi mwingine ni ule wa barabara ya kutoka Kombo - Kifuni hadi kwa Rafaeli inayojengwa kwa fedha za Tozo kwa kiasi cha shilingi milioni 139 miradi mingine ni ujenzi wa madarasa ya mkopo wa kukabiliana na changamoto za UVIKO 19 katika shule za Sekondari Somsom na Manushi ambapo serikali imetoa milioni 100 katika ujenzi wake.
Akiongea na wananchi katika mikutano hiyo, Mbunge aliwahamasisha wananchi wote katika Kata ya Kibosho Magharibi kushiriki katika zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu na kudai kwa takwimu za sensa ni muhimu sana kuwafikishia maendeleo.
Prof. Ndakidemi alitumia mikutano hiyo kueleza wananchi juhudi zinazochukuliwa na serikali kuwaletea maendeleo.
Aliwaambia kuwa kwenye Bajeti ya mwaka wa fedha ya 2022/2023 serikali imetenga fedha za kutosha kusomesha bila kulipa ada watoto wote wa Kitanzania kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, jambo lililoibua furaha kutoka kwa wananchi.
"Hata mtoto ambaye familia yake ina kipato kidogo atapata fursa ya kusoma bila kulipa ada". Alisema mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibosho Magharibi ndugu Nemes Makoi.
Aliwaambia wananchi kuwa serikali kupitia halmashauri itatenga kiasi cha pesa kuwasaidia akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba na kuwaomba kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali waweze kunufaika na fursa hiyo ya mikopo na kumshauri Afisa Maendeleo wa Kata hiyo Nyari kusaidia ili hilo lifanikiwe.
Wakiwasilisha kero zao, wananchi wengi walionyesha kukerwa na miundombinu mibovu ya barabara za ndani zikiwemo zile zote zilizomo kwenye mtandao wa TARURA hasa wakati wa kipindi cha mvua.
Wisema kuwa katika maeneo mengine wakati wa misiba wamekuwa wakilazimika kubeba Majeneza umbali mrefu kwani barabara hazipitiki.
Akijibu kero hiyo, Ndakidemi alisema kuwa tatizo hilo ni sugu katika jimbo lake lote na atalifikisha TARURA.
Alisema kwamba serikali imeendelea kutoa fedha kupitia program mbalimbali kama za Mfuko wa Jimbo wa Barabara, Tozo na matengenezo ya kawaida na kuwaahakikishia wananchi kuwa Rais Samia amedhamiria kujenga miundombinu ya barabara za vijijini.
Kuhusu kero ya uchakavu wa mifereji ya asili na upatikanaji wa umeme na maji safi, Mbunge aliwaomba wana Kibosho Magharibi kuwa wavumilivu kwa kuwa serikali ina nia dhabiti ya kumaliza kero hizo.
Mwakilishi wa TANESCO aliyehudhuria mkutano huo ndugu Freddy Robert alithibitisha kuwa shirika lao litashiriki kikamilifu kutatua kero za umeme katika kata ya Kibosho Magharibi.
Akifunga mikutano hiyo, Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Kibosho Magharibi Nemes Makoi alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea pamoja na Serikali kwa kufadhili miradi mingi ya maendeleo katika kata yake.
Mwisho...
0 Comments