Header Ads Widget

PROF PATRICK NDAKIDEMI (MB) AENDELEA NA ZIARA KWA KUTEMBELEA KATA YA KIBOSHO KIRIMA.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara katika jimbo lake  kwa kutembelea kata ya Kibosho Kirima (alikozaliwa) kukagua  miradi mbalimbali ya Maendeleo na kusikiliza kero za wananchi. 


Mbunge aliongozana na Diwani wa Kata hiyo Inyasi Stoki, Diwani wa viti maalumu Aurelia Mushi, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi wa Kata ya Kibosho Kirima na wataalamu wa serikali kutoka Kata ya Kibosho Kirima.



Kabla ya kwenda kwenye mkutano wa hadhara, Mbunge Ndakidemi alitembelea mradi wa ukarabati wa barabara ya Boro - Sangiti - Kirima KNCU kwa kiwango cha changarawe ambayo iko katika hatua za kukamilika na umetengewa milioni 105. 


Akimkaribisha mbunge kuongea na wananchi, Diwani wa Kata ya Kibosho Kirima, Inyasi Stoki aliainisha mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi kifupi kwa kujengewa na serikali madarasa matano katika shule za sekondari za Kata za Masoka na Kirima kwa gharama ya shilingi milioni 100. 



Mafanikio mengine ni ukarabati wa barabara ya BORO - SANGITI - KIRIMA kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya milioni 105, mradi wa maji wa Maua - Kirima - Boro unakarabatiwa kuongeza kiasi cha maji kwa ufadhili wa milioni 200 kutoka serikali kuu. 


Akiongea na wananchi, Ndakidemi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo katika Kata ya Kibosho Kirima katika sekta ya Elimu, maji, pamoja miundombinu ya barabara, miradi ambayo inatekelezwa kwa kasi na serikali. 



Mbunge Ndakidemi amewataka wana Kibosho Kirima kuendelea kuiamini serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani anafanya makubwa. 


Aidha amewashauri wananchi kutoa ushirikiano wao kwa Rais, Mbunge, Diwani na watendaji wa Serikali ili kufanikisha azma ya kutatua changamoto zinazowakabili bila kujali itikadi za kisiasa. 


Katika mkutano huo, Mbunge aliwashauri wananchi wote wajitokeze Agosti 23 mwaka huu ili wahesabiwe na kudai kuwa takwimu za sensa ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi wa Kata ya Kiboshi Kirima.



"Kujua idadi kamili ya watu na makundi mbalimbali  itarahisisha uandaaji wa mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo" alisema Prof. Ndakidemi.


Wakibainisha changamoto mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kirima juu,  idadi kubwa ya wananchi wameeleza kukerwa na bili kubwa za maji ambazo zimeelekezwa kwa wateja siku za hivi karibuni. 


"Bili za maji ni kero kubwa Mbunge wetu tunaomba hili ulifuatilie pia kitendo cha Jumuiya ya Watumia Maji kusitisha huduma za Vilula vilivyokuwa vinatoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo wa kufungiwa mita za maji hili ni kero" walisema. 


Akichangia hoja katika mkutano huo, Rodrick Shio ambaye ni mkazi wa Kirima juu alionyesha kukerwa na tabia ya ubabe ya uongozi wa vyama vya msingi vya Kimasio na Kirima boro kumpa mwekezaji shamba bila kufuata taratibu na kupata ridhaa ya wamiliki ambao ni Wana Ushirika.


 "Shamba limetolewa kwa mwekezaji bila wamiliki kusema ndiyo au hapana". Alilalamika ndugu Shio na kushangiliwa na mamia ya  wananchi waliohudhuria kwenye mkutano huo. 


Aliendelea, "tunasikia juu juu kuwa yale majengo yanayojengwa ni ya mradi wa kufuga ngombe wazee wetu walinunua lile eneo kwa nia ya kuja kusaidia vizazi vyao kupata maendeleo ya jumla, na sii kama inavyoendelea sasa".


Shio alikuja na hoja hii baada ya Mwenyekiti wa Chama cha  Kimasio John Mliyanga kulaumu viongozi wa kisiasa wa Kata ya Kirima kuwa walisababisha uvunjivu wa amani walipoomba eneo la kujenga Hospitali ya Wilaya na kukataliwa. 


Shio alilaumu kitendo cha viongozi wa vyama vya Kimasio na Kirima boro kugoma kutoa maeneo kwa miradi yenye manufaa kwa maendeleo ya wananchi na Kata ya Kirima. 


Aidha alimwomba mbunge  afuatilie pesa ya SACCOS ya Kirima iliyokusanywa na tume iliyoundwa kukusanya madeni toka kwa wadaiwa sugu. 


Alisema, wana taarifa kuwa zimekusanywa zaidi ya shilingi milioni 8, lakini hazijawasilishwa kwa wahusika.


Aliendelea kudai kuwa kero nyingine ni mapipa mengi ya lami yaliyokuwa katika kata hiyo kuuzwa ambapo Lami hiyo ilikuwa kwenye maeneo mbalimbali ya Kata ya Kibosho Kirima.


Alimwomba mbunge afuatilie ziliko fedha za hiyo lami ili zitumike kwenye miradi ya maendeleo kwenye Kata ya Kibosho Kirima.


Naye mwananchi mwingine, Sisti Mushi wa kijiji cha Kirima Kati alionyesha kukerwa na kasi ya uharibifu wa Mazingira maeneo ya hifadhi kwenye mito yetu. 


Alisema kuwa kuna ujangili unafanyika wa kukata miti aina ya Mikufi kwa kutumia CHAIN SAW. 

"Mheshimiwa Mbunge, ninasikitika kukuarifu kwamba mambo yakiendelea hivi, miti itakwisha huko mtoni tunaomba hatua za haraka zichukuliwe kuwakamata wahusika". Alilalamika Mushi. 


Alisema kwamba yuko tayari kuwasilisha majina ya wahusika kama atatakiwa kufanya hivyo. 


Akijibu hoja za wananchi, Mbunge alionyesha kukerwa na viongozi wa ushirika  wa vyama vya msingi vya Kimasio na Kirima boro wanavyotumia madaraka yao nje ya taratibu, kanuni na sheria za ushirika. 


Aliahidi kulifikisha suala hilo kwa mamlaka husika kwani kwa kiasi kikubwa kiburi cha viongozi wa vyama vya ushirika kimesababisha uvunjivu wa amani. 


"Kule Chama Cha Kirima Boro wanachama waliwaondoa viongozi waliosababisha sintofahamu ya kumilikisha shamba kwa mwekezaji bila ridhaa ya wanachama" alisema Prof. Ndakidemi.


Kuhusiana na kero ya maji, wawakilishi wa RUWASA waliokuwa kwenye mkutano huo  waliahidi kuzifanyia kazi  kero zote zilizowakilishwa na kuwaomba wananchi wenye kero kuziwasilisha ofisini. 


Kuhusiana na Kero ya SACCOS, uharibifu wa miti kwa kutumia CHAIN SAW, na lami iliyouzwa, Mbunge alisema atawasilisha malalamiko hayo kwa mkuu wa wilaya na mamlaka nyingine kwa ufuatiliaji. 


Akifunga mkutano, Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Kibosho Kirima Mwalimu Patrick Mushi alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea pamoja na kuishukuru Serikali kwa kufadhili miraradi mingi ya maendeleo katika kata ya Kibosho Kirima. 


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI